Aina mpya ya corona kutoka Afrika Kusini yafika Kenya

Na  MASHIRIKA

KENYA imegundua visa viwili vya maambukizi ya aina mpya ya virusi vya corona iliyolipuka kwa mara ya kwanza nchini Afrika Kusini, wizara ya afya ilitangaza Alhamisi.

Kaimu mkurugenzi mkuu wa Afya Patrick Amoth Alhamisi alisema kuwa wanaume wawili waliopatikana na virusi hivyo wameondoka nchini Kenya.

Hata hivyo, Dkt Amoth hakuwaambia wanahabari ni wapi wanaume hao walipimwa na ikiwa wamejulishwa kwamba wana virusi hivyo hatari.

“Visa hivi viligunduliwa kutokana na uchunguzi ambao maafisa wetu wanaendesha. Wanaume hawa wawili tayari wamerejea nchini mwao. Wakati ambapo walipatikana, wawili hao hawakuwa wameanza kuonyesha dalili zozote za Covid-19,” akawaambia wanahabari jijini Nairobi.

Wanasayansi wanasema kuwa aina hiyo ya virusi vya corona vinasambaa haraka kuliko vile vya mwanzoni.

Hata hivyo, Dkt Amoth alitoa hakikisho kwamba aina zote za chanjo ambazo zimevumbuliwa kufukia sasa zinaweza kudhibiti aina hii ya virusi vya corona.

Habari zinazohusiana na hii