• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 2:55 PM
FUNGUKA: Utamu wa ubuyu ni ladha tofauti

FUNGUKA: Utamu wa ubuyu ni ladha tofauti

NA PAULINE ONGAJI 

Inapowadia katika masuala ya mapenzi, mara nyingi jamii inamtarajia mtu kuwa na mpenzi mmoja.

Lakini kuna wale wanaopendelea ladha za mahaba kutoka kwa watu tofauti.Lilly ni mmoja wao. Ni mwanamke wa miaka 39, na ni mkazi wa jiji la Nairobi. Anafanya kazi kama mhudumu wa masuala ya mahusiano mema katika shirika moja.

Yeye ni mmoja wa hao wanawake wasiozingatia sana suala la mwonekano na mara nyingi utampata akiwa amevalia tishati, suruali ya jinzi na viatu vya raba.

Aidha, hana mazoea ya kujipaka vipodozi wala kuunda nywele zake.Bibi huyu ameolewa kwa miaka kumi sasa, na pamoja na mumewe, wamejaliwa watoto watatu.

Walifunga ndoa kupitia harusi kubwa ya kanisani.Lakini licha ya kuolewa, Lilly ana wapenzi wengine watatu ambapo wanaume wote wanajuana na kukubaliana na mpangilio wa uhusiano huu, kama anavyosimulia.Mumewe ambaye tutamuita John, ana miaka 44.

Kisha kuna Marco, mwanamume wa miaka 42, ambaye hajawahi oa. Alafu kuna Mika, mwanamume wa miaka 48 ambaye alitalikiana na mkewe miaka mitano iliyopita.

Mpenziwe wa mwisho anaitwa Jack, mwenye umri wa miaka 54, ambaye pia alitalikiana na mkewe.

“Maisha yangu yanaridhisha kwelikweli. Uhusiano huu umekuwa na manufaa mengi kwangu.

Kwanza, kila mwanamume anatimiza mahitaji tofauti; ni kana kila mmoja ana jukumu katika uhusiano huu.Kwa mfano, pamoja na mume wangu John, tunafurahia masuala ya siasa na mahusiano ya kimataifa. Kwa upande mwingine, pamoja na mchumbangu Marco, tunafurahia kutazama filamu.

Tukiwa na mpenzi wangu Mika, tunafurahia masuala ya kidini na kwenda kanisani pamoja, na mwishowe Jack, huwa tunafurahia kambumbu ambapo kila wikendi utatupata katika klabu mbalimbali tukifuatilia ligi za soka za Ulaya.Marco ni stadi wa mahaba ambapo yeye huniacha nikiwa nimeridhika kila wakati.

Lakini haimaanishi kwamba hao wengine hawapati fursa ya kufurahia uhondo huu. Kila mmoja ana nafasi ya kufurahia burudani kuambatana na ratiba tuliyopanga sote pamoja.

Wote wananipenda na hakuna hata mmoja kati yao anayewazia kuwa na uhusiano wa pembeni.Mwanzoni nilipoanza maisha ya kuchumbiana, nilikuwa na wapenzi kadhaa lakini ilikuwa mmoja baada ya mwingine.

Lakini nilipotimu miaka 32 ndipo nilipoanza kukagua sampuli tofauti za madume kwa mpigo mmoja. Hapo ndipo nilipotambua kwamba mimi sio mwanamake anayeridhishwa na mwanamume mmoja bali madume kadhaa, suala ambalo mabinti wengi hushindwa.

Nazungumzia kuhusu uhusiano wangu huu ambao huenda kwa baadhi ya watu sio wa kawaida ili kuwawezesha watu kuwaelewa watu wengine ambao nyoyo zao haziwaruhusu kumpenda mtu mmoja.

Zaidi ya yote, huu ni uhusiano mzuri kwani napata fursa ya kuonja ladha tofauti za mahaba, ndiposa nawahimiza mabinti wengine wajaribu mtindo huu wangu ili wafurahie maisha”.

You can share this post!

Mastaa wa Kenya kujitokeza mbio za Relays zikipamba moto

CHOCHEO: Akikuacha kwenye dhiki utamsamehe ukiomoka?