• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
Mbunge akamatwa kuhusu mapigano Kapedo

Mbunge akamatwa kuhusu mapigano Kapedo

MARY WAMBUI na OSCAR KAKAI

MBUNGE wa Tiaty, Bw William Kamket alikamatwa jana kuhusiana na mashambulio yaliyotokea majuzi eneo la Kapedo ambapo kamanda wa afisa wa kitengo cha GSU aliuliwa.

Mbunge huyo alithibitishia Taifa Leo kuwa alizuiliwa katika kituo cha polisi cha Kileleshwa, kaunti ya Nairobi.

Maafisa wa polisi walikuwa hawajatoa taarifa zozote kwa wanahabari kuhusu kukamatwa kwake kufikia wakati wa gazeti hili kuchapishwa, huku duru zikisema alikuwa amepangiwa kusafirishwa hadi Nakuru.

Mawakili wake na wafuasi waliwasili kituoni lakini polisi wakazuia idadi kubwa ya watu kuingia, wakitaka waingie mmoja mmoja.Baada ya mauaji ya Emadau Tebakol eneo la Kapedo wikendi, Waziri wa Usalama wa Nchi, Dkt Fred Matiang’i alisema kuna viongozi wanaochunguzwa kwa kuchochea na kufadhili vita ambavyo hutokea mara kwa mara katika ukanda huo wa Rift Valley.

Polisi walianzisha oparesheni kali ambapo mnamo Jumatano, watu sita waliuliwa ikisemekana walifyatuliana risasi na polisi.Wakazi katika Kaunti ya Pokot Magharibi jana asubuhi waliandamana katika mji wa Makutano wakipinga oparesheni hiyo.Walisema kuwa watu wasio na hatia wamepoteza maisha na mifugo kuuawa.

Wakiongozwa na diwani maalumu, Bw Elijah Kasheusheu, walimtaka Rais Uhuru Kenyatta kusimamisha oparesheni hiyo na kuruhusu viongozi wao kuwa na mazungumzo kwa ajili ya amani.

“Tumepoteza zaidi ya watu kumi na zaidi ya mifugo 200. Maelfu ya wakazi wamepoteza makao na tunamuomba atusikize,” alisema.Aliongeza kusema kuwa barabara zimefungwa na hakuna pa kupita ili wakazi wapate chakula, dawa na aina nyingine ya misaada wanayohitaji.

You can share this post!

CHOCHEO: Akikuacha kwenye dhiki utamsamehe ukiomoka?

Asimulia alivyotapeliwa kwa jina la Ruto