Wapinzani taabani Ruto akiidhinishwa kuongoza Wakalenjin

Na ONYANGO K’ONYANGO

WAPINZANI wa Naibu Rais William Ruto katika eneo la Bonde la Ufa huenda wakawa na kibarua kigumu kupenya kisiasa, baada yake kuidhinishwa na wazee wa jamii ya Kalenjin kuwa kiongozi wa jamii hiyo.

Baraza la wazee hao, Myoot, limewataka wanasiasa wote katika Bonde la Ufa kumuunga mkono Dkt Ruto anapojiandaa kuwania urais 2022.Wito huo wa Myoot huenda ukawaweka pabaya wanasiasa wa hapo watakaojitokeza kumpinga naibu rais.

“Tunawasihi viongozi wote kumuunga mkono Dkt Ruto ili jamii yetu izungumze kwa sauti moja kabla ya 2022,” akasema mwenyekiti wa Myoot Benjamin Kitur.“Watakaopinga chaguo letu wajipange kwani tutafuatilia mienendo yao kisiasa kwa karibu,” akaongezea.

Tamko hilo la wazee litafanya wanasiasa wanaopinga Naibu wa Rais kukumbwa na upinzani mkali katika maeneo ya Bonde la Ufa.

Wabunge kutoka eneo la Bonde la Ufa wanaochukuliwa kuwa wapinzani wa Dkt Ruto ni Seneta Margaret Kamar, Joshua Kutuny (Cherang’any), Silas Tiren (Moiben), William Chepkut (Ainabkoi), Dkt Swarup Mishra (Kesses) na Gavana wa Elgeyo Marakwet Alex Tolgos.

Katika siku za hivi karibuni, Dkt Ruto amekuwa akizuru maeneo ya Bonde la Ufa mara kwa mara katika juhudi za kuzima uasi. Naibu wa Rais ameunda vikosi vya wafuasi wake ambao watazunguka kote katika eneo hilo wakiendesha kampeni dhidi ya wanasiasa wanaochukuliwa kuwa waasi.

Watakaoendesha kampeni hiyo ni magavana, madiwani na wabunge Oscar Sudi (Kapseret) na Cornelius Serem (Aldai).Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen na mbunge wa Soy Caleb Kositany wametwikwa jukumu la kumtetea Naibu wa Rais Ruto kitaifa.

Bw Serem jana aliambia Taifa Leo kuwa wanasiasa wanaopinga Naibu wa Rais watapoteza viti vyao katika uchaguzi mkuu wa 2022.Alionya baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakieleza wakazi wa eneo hilo kuwa wanaunga mkono Dkt Ruto lakini wakifika jijini Nairobi wanatoa matamshi ya kumdunisha.

“Kiongozi anayepinga Naibu wa Rais katika eneo la Bonde la Ufa ajiandae kumwaga unga 2022. Kundi la wanasiasa waasi linaloongozwa na Bw Kutuny wajiandae kupoteza viti vyao katika Uchaguzi Mkuu ujao,” akasema Bw Serem.

Mbunge wa Keiyo Kusini Daniel Rono aliwataka waasi kujiunga na kambi ya Dkt Ruto kabla ya kampeni dhidi yao kuanza.

“Hatujaanza kampeni dhidi ya waasi, lakini tumeanza kuelezea jamii kujihadhari nao. Hao ni wasaliti wanaofaa kuadhibiwa kwa kunyimwa kura katika uchaguzi ujao,” akasema Bw Rono.M

bunge wa Belgut Nelson Koech alisema kuwa jamii ya Wakalenjin tayari imefanya uamuzi wake kuhusu mwelekeo wa kisiasa hivyo akawataka wapinzani wa Naibu wa Rais kujiandaa kutemwa.

Dkt Ruto ameanzisha juhudi za kumtenga kiongozi wa chama cha Kanu Gideon Moi katika siasa za Bonde la Ufa.Wiki mbili zilizopita, Naibu wa Rais alivutia upande wake kiongozi wa Chama cha Mashinani (CCM) Isaac Ruto ambaye kwa muda mrefu amekuwa mwandani wa Moi.

Habari zinazohusiana na hii

Wachuuzi wa ahadi hewa

Raila amtetea Ruto