• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Mastaa wa Kenya kujitokeza mbio za Relays zikipamba moto

Mastaa wa Kenya kujitokeza mbio za Relays zikipamba moto

Na AYUMBA AYODI

Mastaa wa mbio za mita 100 hadi mita 800 wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi wakati wa duru ya pili ya Mbio za Kupokeza vijiti za kitaifa zitakazoshuhudia vifaa vya kielektroniki vya kurekodi kasi vikitumiwa uwanjani Nyayo jijini Nairobi hapo Jumamosi.

Duru hii imevutia washikilizi wa rekodi za kitaifa Mark Otieno (mita 100) na Hellen Syombua (mita 400) huku wanariadha wakijitahidi kuridhisha kabla ya mchujo wa Riadha za Dunia za Mbio za Kupokezana vijiti.

Tofauti na duru ya kwanza iliyofanyika Januari 9 iliyohusisha mbio zisizo za kawaida za mita 150, mita 300, mita 500, mita 1,000 na mita 1,600, duru ya pili itarejelea mbio za kawaida za mita 100, mita 200, mita 100 kuruka viunzi, mita 400, mita 800 na zile za kupokezana vijiti.

“Tunaweka sawa vifaa ambavyo tutatumia kwenye duru hii,” alisema naibu rais wa Shirikisho la Riadha Kenya (AK) Paul Mutwii, ambaye pia ni mkurugenzi wa mashindano. Mutwii aliongeza kuwa mwanariadha yeyote mtajika anayetumai kuwakilisha Kenya katika Riadha za Dunia za Kupokezana vijiti lazima ashiriki duru ya pili.

Alifichua kuwa baada ya duru ya pili, AK itachagua watimkaji watakaoshiriki duru ya tatu mnamo Februari 6 ambayo itakuwa ya waalikwa pekee.

Mchujo wa kitaifa utaandaliwa Machi 26-27 uwanjani Nyayo. Pia, mchujo huo utakuwa kupitia mwaliko, huku AK ikitayarisha timu itakayopeperusha bendera ya Kenya katika mashindano ya dunia mnamo Mei 1-2 mjini Silesia, Poland.

Otieno, ambaye aliwakilisha Kenya katika Riadha za Dunia za Mbio za kupokezana vijiti mwaka 2019 mjini Yokohama, Japan, alisema atakimbia katika mbio za mita 100 na mita 200, baada ya kukamilisha mbio za mita 150 kwa sekunde 15.5.

“Nilifurahia kutimka mbio za mita 150, ingawa sikuwa nimefanya mazoezi ya kasi msimu huu. Niko tayari kushiriki vitengo viwili msimu huu,” alitangaza bingwa huyo wa Kenya mwaka 2017 na 2018 wa mbio za mita 100. Otieno anashikilia rekodi ya kitaifa ya mbio za mita 100 ya sekunde 10.14.

Amefichua kuwa analenga kukamilisha mbio za mita 100 kwa sekunde 10.05 na zile za mita 200 kwa sekunde 20.23 kabla ya mchujo wa kitaifa na ameomba AK itumie vifaa vya kielektroniki vya kurekodi kasi na vile vya kupima hali ya upepo ili waweze kutimiza ndoto zao. “Tuna ratiba ngumu mwaka huu na itakuwa busara kutumia vifaa hivyo tunapolenga michezo ya Olimpiki,” alisema Otieno.

Ferdinand Omanyala, ambaye alinyakua ubingwa wa mita 300, Dan Kiviasi, Gilbert Osure na Zablon Ekwam ni baadhi tu ya washiriki wa mbio za mita 100 na mita 200.

Zitakuwa mbio za kwanza kwa Syombua tangu akamate nafasi ya nne katika mbio za mita 400 kwenye duru ya Riadha za Dunia za Continental Tour ya Kip Keino Classic mnamo Oktoba 3, 2020.

Syombua atashiriki mbio za mita 400 ambazo zimevutia bingwa wa kitaifa wa mita 400 Mary Moraa, ambaye alitamba katika mbio za mita 500 katika duru ya kwanza, pamoja na Joan Cherono, Veronica Mutua na Sylvia Chesebe, miongoni mwa wengine. – Imetafsiriwa na Geoffrey Anene

  • Tags

You can share this post!

Aina mpya ya corona kutoka Afrika Kusini yafika Kenya

FUNGUKA: Utamu wa ubuyu ni ladha tofauti