• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:05 AM
KALONZO ABURUTA RUTO TOPENI

KALONZO ABURUTA RUTO TOPENI

Na BENSON MATHEKA

Vita vya maneno kati ya Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka kuhusu madai ya unyakuzi wa ardhi na ufisadi, vilichukua mkondo mpya jana baada ya Kalonzo kuwasilisha malalamishi kwa Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Uhalifu (DCI).

Bw Kalonzo anataka Dkt Ruto achunguzwe kwa kueneza habari za uongo dhidi yake, matumizi mabaya ya afisi yake na kutoa matamshi ya uchochezi.

Mnamo Jumatatu, makamu wa rais huyo wa zamani alimlaumu Dkt Ruto kwa kudai alinyakua ardhi ya Idara ya Huduma ya vijana kwa Taifa (NYS) eneo la Yatta, Kaunti ya Machakos.

Alisema matamshi ya Dkt Ruto akiwa Bomet wiki jana yalikuwa ya kumchafulia jina na akaahidi kujiwasilisha kwa DCI na Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) achunguzwe.

Alimtaka Dkt Ruto kujiwasilisha pia ajitakase na kashfa kadhaa alizohusishwa nazo. Jana, Bw Musyoka na mawakili wake, wakiongozwa na maseneta James Orengo na Mutula Kilonzo Junior walifika katika makao makuu ya DCI kuandikisha taarifa kuhusu madai ya Dkt Ruto.

Bw Orengo alisema Bw Musyoka aliwasilisha stakabadhi kuthibitisha kwamba, alifuata sheria kupata ardhi aliyodaiwa alinyakua na ushahidi kwamba matamshi ya Dkt Ruto yalikuwa ya uchochezi.

“Ieleweke kwamba hii sio siasa na haya siyo malalamishi hewa. Ni kuhusu viongozi na maadili. Sheria inafaa kutumiwa dhidi ya viongozi wanaokiuka katiba bila kujali nyadhifa zao,” Bw Orengo alisema.

Alisema Bw Kalonzo anataka Dkt Ruto achunguzwe kwa uchochezi, kutoa matamshi ya uongo na kumchafulia jina.

“Naibu Rais ametenda kosa la uhalifu kwa kutoa matamshi ya kumchafulia jina aliyekuwa makamu wa rais. Hii ni sheria ambayo ni nadra kutumiwa. Hakuna anayeruhusiwa kupaka tope mtu mwingine katika nchi hii kwa kueneza uongo na madai yasiyo na msingi,” Bw Orengo alisema.

Wakili huyo alisema kwamba, matamshi ya Dkt Ruto yalinuiwa kuchochea Wakenya kumchukia Bw Kalonzo.

“Tabia zake ni sawa na za Trump ( aliyekuwa rais wa Amerika,Donald Trump). Lengo lake ni kusababisha migawanyiko katika nchi hii,” aliongeza Bw Orengo.

Alidai kwamba kufuatia matamshi ya Dkt Ruto, Kalonzo na seneta Mutula wamepokea vitisho wasikanyage baadhi ya maeneo nchini.

“Tumewasilisha ushahidi kwa njia ya kielektroniki pia na DCI imeahidi kumuita Naibu Rais kujibu malalamishi yetu,” Bw Orengo alisema.

Bw Kalonzo alisisitiza kuwa mtindo wa maisha wa Dkt Ruto unafaa kuchunguzwa na kwamba Naibu Rais anafaa kujieleza kuhusu madai ya unyakuzi wa ardhi na ufisadi.

“Sisi ni watu wadogo, Wakenya wa kawaida, hatumiliki ndege, ekari 100,000 za ardhi Taita Taveta, au ekari 5,000 Sugoi, hatumiliki mahoteli jijini na hatumiliki sehemu ya uwanja wa ndege wa Wilson kuegesha ndege zetu,” alisema Bw Orengo akigusia baadhi ya sakata ambazo Bw Kalonzo anataka Dkt Ruto achunguzwe dhidi yake.

Ingawa Bw Orengo alisema wanatarajia Naibu Rais kufunguliwa mashtaka katika muda wa wiki tatu, Dkt Ruto ametaja hatua ya Kalonzo kama njama ya kutumia DCI na EACC kumhangaisha kwa kutangaza azima ya kugombea urais 2022.

“Hatutawaruhusu watutishe kupitia DCI na EACC kwamba tusipofanya hivi, watafanya vile. Hii nchi ni yetu sote,” Dkt Ruto alisema.

You can share this post!

Dai serikali ilihadaa kuhusu miradi Boni

Polisi watibua maandamano ya wafuasi wa Bobi Wine jijini...