ODM pia ilaumiwe kwa uzembe wa serikali – Ruto

Wanderi Kamau na DPPS

NAIBU Rais William Ruto  ameambia chama cha ODM kwamba, hakiwezi kamwe kujitenga na uzembe wa serikali ya Jubilee.

Dkt Ruto alisema kwa miaka mitatu iliyopita chama hicho kimekuwa sehemu ya serikali kupitia handisheki na Mpango wa Maridhiano (BBI).

Kwa siku kadhaa sasa, kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, amekuwa akimlaumu Dkt Ruto kwa kuikosoa serikali ya Jubilee kwa kutotimiza ahadi ilizowapa Wakenya, licha ya kuwa ndani yake.

Mnamo Alhamisi, Bw Odinga alimwambia Dkt Ruto ajiuzulu badala ya kuendelea kukosoa serikali ambayo anahudumu kama Naibu Rais.

Hata hivyo, Dkt Ruto amemjibu Bw Odinga akisema ndiye alibadilisha mipango, mikakati na malengo yote ambayo Jubilee ilikuwa nayo baada ya “kuingia” serikalini.

“Ulikuja na kubadilisha mipango ya serikali kama Ajenda Nne Kuu za maendeleo, ukaleta BBI. Baada ya juhudi zako kukosa kufaulu, unataka kutoroka. Lazima ubebe lawama za Jubilee kutotimiza ahadi zake. Huwezi kuendelea kulaumu wengine,” alihoji nyumbani kwake Karen, Nairobi.

Dkt Ruto alitoa kauli hiyo jana wakati akiwahutubia madiwani kutoka Kaunti ya Mandera waliomtembelea kwenye makazi yake mtaani Karen, jijini Nairobi.

Habari zinazohusiana na hii

HASLA BANDIA

Ruto ainua mikono

Ruto akatwa mbawa