• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 9:55 AM
Dai serikali ilihadaa kuhusu miradi Boni

Dai serikali ilihadaa kuhusu miradi Boni

Na KALUME KAZUNGU

SERIKALI ya kitaifa imelaumiwa kwa kutokamilisha miradi mikuu iliyokuwa imepangwa kutekelezwa kwenye maeneo ambako operesheni ya usalama ya Linda Boni inaendelezwa, Kaunti ya Lamu.

Licha ya serikali kutangaza kutumia zaidi ya Sh50 bilioni katika kuendeleza operesheni ya Linda Boni kwenye msitu wa Boni, wakazi wanalalamika kuwa miradi mingi waliyoahidiwa kwamba ingetekelezwa bado imebakia kuwa ndoto.

Mnamo Septemba, 2015, serikali kuu ilizindua operesheni ya usalama ya Linda Boni, dhamira kuu ikiwa ni kuwafurusha au kuwamaliza magaidi wa Al-Shabaab wanaoaminika kujificha ndani ya msitu wa Boni.

Serikali pia ilikuwa imeahidi kwamba ingejenga barabara, kukarabati shule, viwanja vya ndege, kuwachimbia wakazi visima na hata kuwapa chakula msimu wote ambapo operesheni hiyo ingetekelezwa.

Utafiti uliofanywa na Taifa Leo kwenye vijiji mbalimbali ambako operesheni ya Linda Boni inaendelea ulibaini kuwa miundomsingi maeneo hayo bado ni duni.

Mwakilishi wa Wadi ya Basuba, ambaye pia ni msemaji wa Jamii ya Waboni, Barissa Deko aliuliza serikali zilikokwenda Sh50 bilioni za Operesheni ya Linda Boni, ikizingatiwa kuwa miundomsingi eneo lao bado ni ya kusikitisha.

“Wanasema walitumia Sh50 bilioni katika shughuli za operesheni ya Linda Boni. Fedha hizo zilienda wapi kwani barabara, shule na miundomsingi mingine bado iko katika hali duni? Waboni wanateseka kwa kukosa maji. Madarasa kwenye shule zetu za Bodhai, Pandanguo, Milimani, Basuba, Mangai, Mararani na Kiangwe yana nyufa. Hatuna madawati. Serikali ijukumike kuinua miundomsingi eneo letu,” akasema Bw Deko.

Bi Hawa Abdi alisema wanawake kwenye vijiji vya Waboni hurauka kila siku na kutembea mwendo mrefu wakitafuta maji.

Bi Abdi alisema licha ya serikali kuahidi kuchimba visima eneo lao, ahadi hiyo bado haijatimizwa.

Aliisihi serikali kuacha kucheza na maisha ya mwananchi na kuhakikisha wananchi wanaoishi kwenye maeneo ya operesheni wanainuliwa kimiundomsingi.

“Wanawake hapa msitu wa Boni tumechoka kutembea zaidi ya kilomita 20 tukitafuta maji kila siku. Watuchimbie visima kama walivyotuahidi miaka saba iliyopita,” akasema Bi Abdi.

Wakazi pia waliishinikiza serikali kukarabati barabara na viwanja vya ndege eneo hilo ili kurahisisha usafiri, ikiwemo ule wa maafisa wa usalama eneo lao.

Bw Ahmed Salim alisema wamechoka kutumia fedha nyingi wakisafiri kwa kutumia boti na mashua baharini.

Kwa upande wake aidha, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia, alishikilia kuwa serikali inafanya kila jitihada ili kuboresha miundomsingi na maisha ya wakazi kwa jumla kwenye maeneo yote ambako oparesheni ya Linda Boni inaendelezwa.

“Hivi majuzi nilikuwa kwenye kivuko cha Kwa Omollo kilichoko msitu wa Boni. Tunajikakamua kuona kuwa kivuko hicho na pia barabara ya Witu hadi Pandanguo vinakarabatiwa. Wananchi wasiwe na shaka,” akasema Bw Macharia.

You can share this post!

UMBEA: Mwanamke huridhishwa zaidi na ukarimu na upendo wa...

KALONZO ABURUTA RUTO TOPENI