• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:03 PM
DINI: Unapotubu na kuungama, Mungu mwenye rehema atakufuta machozi na kukunusuru

DINI: Unapotubu na kuungama, Mungu mwenye rehema atakufuta machozi na kukunusuru

NA PADRE FAUSTIN KAMUGISHA

WANADAMU kuna mengi tunayokumbana nayo. Kama inavyosema Biblia katika kitabu cha Mhubiri 3:1-8, “Kwa kila jambo, kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu”.

Kuna wakati wa kuzaliwa na wakati wa kufa. Wakati wa kupanda na wakati wa kung’oa yaliyopandwa. Wakati wa kuua na wakati wa kupoza. Wakati wa kubomoa na wakati wa kujenga.

Kuna wakati wa kulia na wakati wa kucheka. Wakati wa kuomboleza na wakati wa kucheza. Wakati wa kutafuta na wakati wa kupoteza. Wakati wa kuweka na wakati wa kutupa.

Kuna wakati wa kurarua na wakati wa kushona. Wakati wa kunyamaza na wakati wa kunena. Wakati wa kupenda na wakati wa kuchukia. Wakati wa vita na wakati wa amani.

Hata hivyo, wakati wa kuomboleza huwa mgumu mno. Kuna hali nyingi zinazotufanya kulia.

Jambo la kwanza ni dhambi. Wakati mwingine Mungu huruhusu tupitie hali ngumu kwa sababu ya dhambi zetu. Mshahara wa dhambi ni mauti na kila kosa sharti liadhibiwe.

Hiyo ndiyo sababu ilimpasa Yesu Kristo afe ili kwa kumwamini tusamehewe.

Hata hivyo sio mateso yote husababishwa na dhambi. Mengine huja ili Mungu ajitukuze (Yohana 9:1-7).

Kilio na mateso pia huja kwa lengo la kuturekebisha. Tunapoziacha njia za Mungu tunaweza kupitia hali ya majonzi tele. Lakini tunapotambua makosa yetu na kumrejea, ana rehema nyingi, anatusamehe na kuturejeshea furaha.

Mungu ni mzazi mwema na anamtaka kila mmoja wetu akomae. (Waebrania 12:7-13). Vile vile, mateso huja ili kujaribu imani yetu. Mateso yanajenga imani yetu na kutufanya tumtumikie Mungu vyema.

Kupitia kwa magumu, Mungu anatuteng’eneza na kutugeuza kuwa Baraka kwa wengi. “Na Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatia nguvu,” maandishi matakatifu yasema.

Wanadamu na nguvu za giza pia huinuka kinyume na Wakristo na kuwasababisha kuwa na kilio. Vita tunayopigana si vya damu na nyama. Kuna nguvu za ushirikina na uchawi ambazo huinuka kuzuia maendeleo yako.

Ndio sababu kama Mkristo, unapaswa kuomba bila kukoma. Usiyachukulie mambo hivi hivi. Omba kwa bidii ili uvunje na kuharibu mipango yote ya giza dhidi ya maisha yako.

Katika kilio chako kuna matumaini, maana kunaye Mungu anayesikia kilio chetu. Wana wa Israeli walipokuwa Misri palitokea Farao asiyemjua Yusufu.

Hapo mambo yakabadilika. Watu waliokuwa matajiri na kuishi katika nchi ya utele, wakajipata wamefanywa watumwa na wakaanza kupitia mateso makali.

Mateso yalipozidi walilia! Si vibaya kulia. Mambo yakizidi, lia! Mungu alisikia kilio chao.

Kitabu cha Kutoka 3:7,8 kinasema hivi: “Bwana akasema, hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walio Misri. Nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao, maana nayajua maumivu yao. Nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile hadi nchi njema, iliyojaa maziwa na asali.”

Cha ajabu ni kuwa, Waisraeli hawakuwa wanamlilia Mungu. Walikuwa wanalia kwa sababu ya mateso yao. Lakini Mungu alisikia kilio chao.

Mateso unayoyapitia, Mungu anayaona! Kilio chako, Mungu anakisikia. Kama aliwasikia wana wa Israeli na hawakuwa wanamlilia, sembuse wewe unayemlilia moja kwa moja?

Usiwalilie wanadamu, hawana msaada kwako. Mlilie Mungu naye atakuokoa na mazito yote unayoyapitia. Zaburi 34:17 inaeleza: “Wenye haki walilia, naye Bwana akasikia, akawaponya na taabu zao zote.”

Mambo tunayoyapitia ni kwa muda tu. Usikate tamaa. Mungu anaona mateso yako na ana mpango mwema nawe. Zidi kumwamini na kumtegemea katika kila hali.

Hatimaye utatokea kuwa mshindi. Wewe si mshindwa. Hatima yako ni ushindi mkubwa. Ufunuo 21:4,5 inasema: “Naye atafuta kila chozi katika macho yao; wala mauti haitakuwapo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu. Kwa kuwa mambo ya kale yamekwisha kupita.

“Na yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi akasema: Tazama, nayafanya yote kuwa mapya. Akaniambia, andika ya kwamba maneno hayo ni amini na kweli.”

You can share this post!

Viongozi wataka Jaji Mkuu mpya ateuliwe kwa uwazi

Wakazi Pwani walalama kuuziwa nyumba bila ardhi