• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Wakazi Pwani walalama kuuziwa nyumba bila ardhi

Wakazi Pwani walalama kuuziwa nyumba bila ardhi

Na PHILIP MUYANGA

HEBU tafakari haya; unavutiwa na nyumba, ukachukua mkopo na kuilipia.

Unapojiandaa kutwaa umiliki wake, aliyekuuzia anakukumbusha kuhusu sharti moja ambalo ni la kutamausha: Ndio, alikuuzia nyumba lakini si ardhi ilikojengwa nyumba yenyewe. Yote hayo ni kama ngano ila hayo ndiyo masaibu wanayopitia wakazi wa Pwani.

Wakazi hao wanatakiwa kulipa Sh300 kila mwezi kwa wanaowazuia kama kodi ya ardhi ambayo nyumba imejengwa. Hii ni tofauti na maeneo mengine ambapo mtu akinunua nyumba huwa anamiliki sehemu ya ardhi ilikojengwa.

Mfumo unaotumiwa maeneo ya pwani umeacha wataalamu wa ardhi, wanasheria na majaji katika mshangao kuhusu ulivyoanza na jinsi wakazi wanavyoutekeleza.

Mfumo huo wa nyumba bila ardhi umekuwa ukitekelezwa eneo hilo kwa muda mrefu.

Mtu anayetaka kujenga nyumba huwa analipa kati ya Sh300,000 na Sh1 milioni kwa mwenye ardhi kabla ya kutia saini mkataba.

Baada ya kupata ploti, anayetaka kujenga nyumba hutakiwa kulipa mmiliki wa ardhi Sh300 kila mwezi akimaliza kujenga nyumba.

Hata hivyo, wakazi wengi huwa wanakataa kulipa ada hizo baada ya malipo ya kwanza wakisema zinatosha.

“Nilinunua kipande cha ardhi na kulipa pesa, nilijenga nyumba yangu lakini nikakataa kulipa kodi ya ploti,” alisema mkazi mmoja wa Likoni ambako mfumo huu unatumiwa sana.

Mkazi huyo aliyeomba tusitaje jina ili asidhulumiwe na aliyemuuzia ardhi alisema, watu wengi wamenunua ploti lakini hawana stakabadhi halali za kuthibitisha wanazimiliki.

Mkazi mwingine wa Mombasa, Bw Mohamed Mohamed, alisema alikubaliana na mwenye ardhi akanunua ploti na sasa anatakiwa kulipa Sh250 kila mwezi kama kodi ya ploti.

“Sina shida na mfumo huu, wengi wetu tunafahamiana, nililipa pesa hizo na nikapewa ploti yangu,” alisema Bw Mohamed.

Alisema haoni shida ya kulipa kodi ya ardhi kila mwezi.

Haijulikani mpango huo ulianzia wapi lakini baadhi ya wanahistoria wanahusisha na utawala wa Sultan wa Zanzibar aliyetawala eneo la pwani kabla ya Kenya kupata uhuru.

Mpango huo wa nyumba bila ardhi unatumiwa sana maeneo ya Kisauni, Likoni na sehemu za kaunti za Kwale na Kilifi.

You can share this post!

DINI: Unapotubu na kuungama, Mungu mwenye rehema atakufuta...

Washirika wa Ruto wapuuza kutawazwa kwa Moi