Watamjaribu Baba?

Na BENSON MATHEKA

CHAMA cha ODM kimealika wanaomezea mate tikiti ya kuwania urais kwa chama hicho, na kuzua maswali iwapo yupo atakayethubutu kushindana na kiongozi wake, Raila Odinga.

Kinara huyo ambaye yuko kwenye ushirikiano wa handisheki, amekuwa mgombea urais wa ODM tangu chama hicho kilipoundwa 2007.

Baadhi ya wanachama waliowahi kuelezea nia ya kuwania mchujo wa urais ni magavana Hassan Joho (Mombasa), Wycliffe Oparanya (Kakamega) na Amason Kingi (Kilifi).

Magavana wote watatu wanahudumu muhula wao wa mwisho kikatiba na hawaruhusiwi kuwania tena ugavana. Kwa hivyo, wanaruhusiwa kuwania urais. Hata hivyo swali lililo vinywani mwa wengi ni iwapo watakuwa na ujasiri wa kuwasilisha maombi ya kumenyana na Bw Odinga katika kutafuta tiketi ya kupeperusha bendera ya ODM kwenye debe mwaka ujao.

Kupitia ilani iliyotolewa na Bodi ya Uchaguzi ya chama hicho, chama cha ODM kinataka walio na azima ya kugombea urais kutuma maombi yao kufikia Februari 26.

Mwenyekiti wa bodi ya uchaguzi, Bi Catherine Mumma, kwenye tangazo magazetini jana alisema, hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya ODM kuendeleza mipango ya kujiandaa kwa uchaguzi mkuu.

Kufikia sasa, Naibu Rais Dkt William Ruto, Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara (UNCTAD), Dkt Mukhisa Kituyi na Gavana wa Makueni Prof Kivutha Kibwana ni kati ya wale wameshatangaza hadharani nia ya kuwania urais.

Lakini Bw Odinga hajatangaza hadharani iwapo atawania au la, huku akisema kampeni ya kupigia debe marekebisho ya Katiba kupitia BBI haina uhusiano wowote na uchaguzi wa urais.

Bi Mumma kwenye wito wa maombi kutoka kwa wanachama alisema, wanaotaka kuwania urais kwa tiketi ya ODM ni lazima wawe watu wa maadili ya hali ya juu na tabia njema katika jamii.

“Wanaotuma maombi ni lazima watimize masharti yote ya sheria na kanuni za uchaguzi za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC),” Bi Mumma alisema kwenye tangazo magazetini.

Alisema wawaniaji ni lazima wawe wanachama wa maisha ambao wamedhihirisha kujitolea kwa vitendo kutekeleza ajenda za chama cha ODM.

“Wanaotafuta urais kupitia ODM ni lazima wawe watu wa maadili mema na nidhamu ya hali ya juu,” alisema Bi Mumma.

Pia wanapaswa kuwa wapigakura waliosajiliwa nchini Kenya, walio na digrii kutoka chuo kikuu kinachotambuliwa nchini Kenya na waliohitimu kugombea kiti cha ubunge.

Wanaotuma maombi ni lazima waambatishe hati ya kiapo wakithibitisha kwamba stakabadhi na habari kuwahusu ni za kweli.

Aidha, ni lazima walipe ada ya Sh1 milioni kwa chama kabla ya Februari 26, tarehe ya mwisho ya kupokea maombi.

“Wanaotuma maombi ni lazima waambatishe ushahidi kwamba wamelipa Sh1 milioni kwa akaunti ya benki ya chama cha ODM,” alieleza Bi Mumma.

Alisema ada hiyo haitarudishwa iwapo anayetuma ombi hatakabidhiwa tiketi ya chama hicho kugombea urais.

Ingawa Bw Odinga hajajitokeza peupe kutangaza nia yake ya kuwania kiti hicho kwa mara ya tano, kuna kila ishara, hasa kutokana na matamshi ya washirika wake wa karibu, kwamba atakuwa kwenye debe mwaka ujao.

Habari zinazohusiana na hii

ODM: Raila anachezwa

Kingi amzima Raila

Kichwa kinauma

Raila akausha marafiki