• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:21 PM
Washirika wa Ruto wapuuza kutawazwa kwa Moi

Washirika wa Ruto wapuuza kutawazwa kwa Moi

Na ERIC MATARA

VIONGOZI wanaumuunga mkono Naibu Rais William Ruto katika eneo la Rift Valley, Jumapili walipuuzilia mbali kutawazwa kwa seneta wa Baringo, Gideon Moi kuwa mzee wa Wakalenjin na msemaji wa jamii hiyo.

Viongozi hao, akiwemo mbunge maalumu Gideon Keter, Nelson Koech (Belgut),Kimani Ngunjiri(Bahati) Aaron Cheruiyoit (Seneta, Kericho na Samson Cherargei (Seneta, Nandi) walisema kwamba msemaji wa jamii hiyo ni Dkt Ruto.

“Kiongozi wetu na msemaji wa eneo la Rift Valley ni Naibu Rais William Ruto. Seneta Moi anataka kutumia kutawazwa kwake kufanya biashara katika siasa,” alisema Bw Keter.

Wanasiasa hao walisema kutawazwa kwa Seneta Moi kunalenga kupotosha watu kuamini kwamba anaungwa mkono Rift Valley.

“Eneo lote la Rift Valley,linohusisha jamii za Kalenjin, Wamaasai, Waturkana na Wasamburu, liko nyuma ya Dkt Ruto na yeyote anayempinga anapoteza wakati. Tutampigia kura kwa wingi 2022 na tutamuunga mkono amrithi Rais Uhuru Kenyatta,” alisema Seneta Cheruyoit.

Walisema kwamba Dkt Ruto hawezi kushindana kisiasa na seneta Moi.

“Naibu Rais Ruto ndiye maarufu Rift Valley na katika kampeni za kumrithi Rais Kenyatta. Hawezi kuanza kushindana na watu kama seneta Moi,” alisema Bw Keter.

“Dkt Ruto ndiye aliyeongoza kampeni za Rais Uhuru Kenyatta kwenye uchaguzi wa 2013 na 2017.

Pia aliongoza kampeni za aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa 2007 na kwa hivyo umaarufu wake sio wa kubahatisha,” aliongeza.

Seneta Moi ambaye ni mwenyekiti wa Kanu alitawazwa kuwa mzee wa Wakalenjin na msemaji wa jamii hiyo na kundi la wazee wa Talai wiki tatu baada ya vijana waliohusishwa na Dkt Ruto kuzima hafla iliyopangwa kufanyika Kapsisiywa kaunti ya Nandi.

Vijana hao walifunga njia iliyoelekea Kapsisiywa na kumfanya seneta Moi kukatiza mipango ya kufika huko.

Mnamo Ijumaa, kundi la wazee hao lilimkabidhi nyenzo za uongozi vya jamii hiyo na kumtwika jukumu la kugombea kiti cha uongozi wa nchi.

You can share this post!

Wakazi Pwani walalama kuuziwa nyumba bila ardhi

Wandani wa Uhuru wamsuta Ruto kuhusu BBI