Wandani wa Uhuru wamsuta Ruto kuhusu BBI

Na WAWERU WAIRIMU

VIONGOZI wanaomuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta wamemshutumu Naibu Rais William Ruto dhidi ya kuwapotosha vijana walalahoi kwa kuwapa matumaini ya uongo, kupitia simulizi ya wilbaro badala ya kuinua maisha yao kupitia miradi ya maendeleo na kuwaimarisha.

Viongozi hao kutoka Isiolo, Baringo na Nairobi walipuuzilia mbali siasa za Mahasla na Dynasty na kuwashutumu viongozi wa mrengo wa Tangatanga unaomuunga mkono Naibu Rais dhidi ya kutumia siasa hizo kuendeleza ajenda za kibinafsi badala ya kuwaunganisha Wakenya.

Mwakilishi Mwanamke Kaunti ya Baringo Gladwell Cheruiyot alisema lengo kuu la ripoti ya BBI ni kuimarisha Katiba iliyopo sasa kuwaunganisha Wakenya, kuhakikisha ujumuishaji na kumaliza ghasia za uchaguzi ambazo zimeshuhudiwa awali, kwa kuwezesha maendeleo kote nchini.

Wabunge hao walisisitiza haja ya uongozi wa taifa kubaki na umoja na kuwahimiza Wakenya kutojiunga na siasa za Mahustler akisema “hakuna anayependa kuwa maskini.”

Mbunge wa Starehe Charles Kanyi (Jaguar) alisema Dkt Ruto anawatumia vibaya vijana ambao hawajaajiriwa kupigia debe siasa za Hustler na kuitisha hatua ya dharura ili kuangazia suala hilo.

“Naibu Rais anatumia vibaya pengo hilo na ni sharti tuketi chini na vijana na kujua tatizo liko wapi ili litatuliwe nao wasipotoshwe,” alisema Mbunge huyo.

Alisema serikali kando na ajira rasmi inapaswa kuwapa vijana mtaji na nafasi ili waanzishe biashara zao binafsi na kujiimarisha.

Bw Jaguar aliwahimiza Wakenya kusoma nakala ya BBI na kuielewa vyema ili wasipotoshwe na kuwataka viongozi kote nchini kuungana pamoja ili mchakato huo uendelee shwari.

Akizungumza katika mkutano wa kuhamasisha kuhusu BBI mjini Isiolo ulioandaliwa na chama cha KANU, Gavana wa Isiolo Mohamed Kuti na Seneta Mteule Abshiro Halake walisema wanaunga mkono kikamilifu BBI na serikali inayotawala.

Dkt Kuti na Spika wa Isiolo Hussein Roba hata hivyo walitofautiana na mpango wa ugavi wa mapato kwa misingi ya idadi ya watu, ambao utapunguza kiwango cha fedha zinazotengewa eneo la Kaskazini, na kuwahimiza Rais Kenyatta na Bw Odinga kuruhusu marekebisho ili maendeleo zaidi yawezeshwe katika eneo hilo.

“Tumo katika treni ya BBI na tutaunga mkono mchakato huo huku tukiitisha mabadiliko machache ili isinufaishe tu kaunti zilizo na idadi kubwa ya watu na kuathiri kaunti chache zillizo na idadi ndogo ya watu. Maeneobunge yaliyoongezwa yanapaswa kugawanywa miongoni mwa kaunti 47,” alisema Dkt Kuti.

Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Wazee Phares Rutere alisema Wakenya wanapaswa kuelimishwa kikamilifu kuhusu ripoti ya BBI akisema wengi wao hawajasoma nakala hiyo hivyo basi haimaanishi haiungwi mkono.

Alihimiza jopokazi la BBI kuwateua wazee watakaoongoza shughuli ya kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa ripoti hiyo.

“BBI ni nzuri na itaimarisha ugatuzi na kuhakikisha maendeleo zaidi. Idadi kubwa ya Wakenya hawajasoma ripoti hiyo na hilo halimaanishi haina umaarufru,” alisema Bw Rutere.

Alimhimiza Gavana Kuti kuunda jopokazi la kaunti ili lisaidie katika kuelimisha umma mashinani.

Mwanasiasa Maina Njenga aliunga mkono marekebisho ya katiba akisema hatua ya kuongeza fedha zinazotengewa kaunti itahakikisha maendeleo katika wadi.

Habari zinazohusiana na hii

Uhuru aomba talaka

Watermelon mpya?

BBI: Ruto atapatapa

Mambo yaenda segemnege