• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
Pigo Man-City na Leicester masogora tegemeo De Bruyne na Vardy wakitarajiwa kusalia mkekani kwa muda mrefu

Pigo Man-City na Leicester masogora tegemeo De Bruyne na Vardy wakitarajiwa kusalia mkekani kwa muda mrefu

Na MASHIRIKA

KIUNGO Kevin de Bruyne wa Manchester City na mshambuliaji Jamie Vardy wa Leicester City watasalia mkekani kwa kipindi kirefu kijacho ili kuuguza majeraha.

Kwa mujibu wa kocha Pep Guardiola wa Man-City, De Bruyne, 29, anatarajiwa kuwa nje kwa kipindi cha kati ya wiki nne na sita kuuguza jeraha la paja alilolipata kwenye mchuano wa EPL uliowakutanisha na Aston Villa mnamo Januari 20, 2021.

Man-City walisajili ushindi wa 2-0 katika mechi hiyo na kupaa hadi nafasi ya pili jedwalini kwa alama 38 sawa na Leicester waliotawazwa mabingwa wa EPL kwa mara ya mwisho mnamo 2015-16 chini ya mkufunzi Claudio Ranieri. Ni pengo la alama mbili pekee ndilo kwa sasa linawatenganisha Man-City na viongozi wa jedwali Manchester United.

De Bruyne anatazamiwa kukosa mechi 10 zijazo za Man-City, ikiwemo ile ya mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) dhidi ya Borussia Monchengladbach mnamo Februari 24.

“Daktari amemetathmini De Bruyne na kupendekeza kwamba asalie nje kwa kati ya wiki nne na sita. Ni pigo kubwa kwa Man-City,” akasema Guardiola.

Hadi walipovaana na Cheltenham Town kwenye raundi ya nne ya Kombe la FA mnamo Januari 24, Man-City hawakuwa wameshindwa katika mechi 16 zilizopita katika mapambano yote ya msimu huu.

Baada ya kukosa mechi iliyokutanisha Man-City na Cheltenham, De Bruyne atakosa pia mechi zijazo za EPL zitakazokutanisha waajiri wake na West Brom, Sheffield United, Burnley, Liverpool, Tottenham Hotspur, Arsenal, West Ham na Manchester United.

Kwa upande wake, Vardy ambaye anatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa kinena katika kipindi cha wiki chache zijazo, atakuwa nje kwa hadi wiki tano.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 34 anajivunia mabao 11 ya EPL hadi kufikia sasa na amesaidia Leicester kusalia miongoni mwa wagombezi halisi wa taji la msimu huu.

Kutokuwepo kwa Vardy kunatarajiwa kumweka kocha Brendan Rodgers katika ulazima wa kutegemea zaidi maarifa ya mafowadi Ayoze Perez na Kelechi Iheanacho watakaoshirikiana na viungo wavamizi Harvey Barnes na James Maddison.

You can share this post!

Tshisekedi azidi kuudhibiti usemi wa Kabila serikalini

Wakazi wa Kilifi walalamika kutembea kilomita 10 kutafuta...