• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
Serikali yatakiwa kuwapa walimu ulinzi wa kutosha

Serikali yatakiwa kuwapa walimu ulinzi wa kutosha

EVANS KIPKURA na STEVE NJUGUNA

MUUNGANO wa walimu nchini umetoa wito kwa serikali kurejesha amani katika kaunti za Bonde la Ufa ambazo zinakumbwa na visa vya wizi wa mifugo na uharamia.

Walimu katika kaunti za Baringo, Samburu, Turkana na Elgeyo Marakwet wamesema maafisa wa muungano huo bado hawajarejea shuleni kwa sababu ya visa vya uharamia vinavyozidi kuongezeka katika sehemu hizo.

Msururu wa mashambulizi yaliyoshuhudiwa majuzi katika eneo la Tiaty na kaunti zinazopakana na Elgeyo Marakwet, Samburu na Pokot Magharibi, yametatiza shughuli za masomo.

Miungano hiyo sasa inaomba serikali kutilia maanani wajibu wake wa kuwapa raia wake ulinzi katika mazingira kama hayo.

“Hali inayoshuhudiwa Kapedo ni ya kuhuzunisha mno. Imeenea hadi katika kaunti jirani na kuzorotesha shughuli za masomo kote. Hii ni kwa sababu hakuna mwalimu yeyote aliye na ujasiri wa kufanya kazi mahali ambapo usalama wake unatishiwa,” alisema Bw Omboko Milemba, ambaye ni mwanachama wa Bunge la Kitaifa na mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha walimu cha KUPPET, wakati wa uchaguzi wa muungano huo tawi la Iten.

Bw Milemba alisema kwamba atawasilisha mswada bungeni kushinikiza walimu wapewe ulinzi na serikali kila mara mashambulizi yanapozuka.

Viongozi hao walisema iwapo serikali haitahakikisha kwamba kuna usalama katika maeneo yaliyoathirika, watawashauri walimu wasirejee kazini kabisa.

“Pasipo usalama haiwezekani kabisa kwa walimu kutekeleza majukumu yao. Serikali inapaswa kuhakikisha usalama wa walimu unaimarishwa kote nchini.

“Tunahofia kwamba endapo mapigano yataendelea Baringo, Samburu na Marakwet, hakuna mwalimu atakayeenda darasani,” alisema Naibu Mwekahazina wa chama kingine cha walimu KNUT, Bw James Mugo Ndiku, alipoongoza chaguzi za muungano wa walimu tawi la Keiyo.

Wakati huo huo, KUPPET imehimiza Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) kuhamisha wale ambao wameshambuliwa na wanafunzi, katika siku za hivi majuzi.

Muungano huo ulilalamikia ongezeko la visa vya wanafunzi kushambulia walimu nchini, ukisema kwamba njia pekee ya walimu walioathirika kuepuka unyanyapaa ni kwa wao kuhamishwa kutoka shule husika.

“Mwalimu anaposhambuliwa na mwanafunzi hawezi tena kusimama mbele ya wanafunzi hao na kuwafunza vyema. Ndiposa tunahimiza TSC kutilia maanani ombi la kuhamisha walimu husika ili waepuke kudhalilishwa,” alisema Katibu Mkuu wa KUPPET tawi la Laikipia, Bw Robert Miano.

Alitaja kisa ambapo mwalimu alishambuliwa na mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari ya Murichu, mjini Ndaragwa.

Bw Miano alisema iwapo TSC itakosa kumhamisha mwalimu huyo, basi atafanyiwa dhihaka na wanafunzi katika shule hiyo.

“Mwalimu alishambuliwa na mwanafunzi mbele ya wanafunzi wote. Ni rahisi kwake kugeuzwa dhihaka; wanafunzi watamkosea heshima. Njia pekee ya kuepuka hali hiyo ni kumhamisha,” akasisitiza.

Kiongozi huyo wa walimu alitoa wito kwa Wizara ya Elimu kuanzisha mpango masuala ya kijamii ili wanafunzi wapewe ushauri nasaha kuzima utundu miongoni mwao.

You can share this post!

Watamjaribu Baba?

Suala la kukuza miwa bondeni laibua mzozo