TAHARIRI: Dawa za nguvu za kiume zidhibitiwe

KITENGO CHA UHARIRI

SUALA la matumizi ya dawa za kuongeza nguvu za kushiriki mapenzi, linahitaji mjadala wa kitaifa, ili kuepusha jamii kuangamizwa na utumzi mbaya wa dawa hizo.

Japokuwa lilianza kama uvumi, imebainika kuwa kweli kuna wanaume ambao wamefariki dunia baada ya kutumia vidonge vya kuwaongeza ashiki. Dawa hizo ambazo hupatikana kwa njia rahisi kwenye maduka ya dawa, sasa zimekuwa njia rahisi zaidi ya mauti, hata kushinda maradhi hatari.

Kinachosikitisha ni kwamba, hata baada ya watu kusikia habari za wenzao kufa kwenye magesti, uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo umeonyesha kuna ongezeko kubwa la wanaume wanaozitafuta.

Wasichofahamu ni kwamba dawa hizo zinazofahamika kwa majina mengi likiwemo la Viagra, husaidia kusukuma damu kwa kasi. Msukumo huo ukiongezwa na nguvu zinazotumika, humfanya mtu kuwa kama aliyekimbia masafa ya mbio za Eliud Kipchoge. Katika maisha halisi, wanaume wengi huwa hawafanyi mazoezi ya kwenda kasi au urefu kama huo.

Wataalamu wa afya wanasema jambo hilo ni hatari, kwa kuwa damu huchemka kupita kiasi na kuna uwezekano mkubwa wa kupasuka mishipa muhimu, kama vile ya kwenye moyo au ubongo na kusababisha kifo.

Kinachohitajika sasa ni mazungumzo wazi kutoka kwa maafisa wa wizara ya Afya kuhusu madhara ya kutumia dawa hizi.

Serikali yapaswa kuanzisha kampeni sawa na ya kudhibiti maambukizi ya corona. Watu wahimizwe kufanya mazoezi, wale vyakula asili na wasijihusishe na vitendo vinavyoweza kuchangia kupungua kwa nguvu za kiume.

Viongozi wa kidini wahamasishe waumini kuhusu amri za kujiepusha na kushiriki mapenzi nje ya ndoa. Takwimu zote kufikia sasa zinaonyesha waliofariki kwenye tendo hilo hawakuwa katika nyumba zao. Ina maana kuwa walitumia dawa hizo kuonyesha ushujaa usiokuwa na maana kwa afya zao.

Bunge lina jukumu la kubuni kanuni za kudhibiti uuzaji na usambazaji wa dawa hizo. Hata kama kweli wanaume wanazihitaji, iwapo zitakuwa hazipatikani kwenye maduka ya dawa, basi hawatazinunua.

Mojawapo ya kanuni hizo iwe ni kuruhusu kuuzwa kwa dawa za kuongeza nguvu za kiume kupitia barua ya daktari pekee. Daktari atakuwa amempima mgonjwa na kuelewa hali yake ya kiafya kama presha, sukari, kati ya maradhi mengine.

Habari zinazohusiana na hii