• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Chelsea wamtimua kocha Frank Lampard baada ya miezi 18

Chelsea wamtimua kocha Frank Lampard baada ya miezi 18

Na MASHIRIKA

CHELSEA wamemfuta kazi kocha Frank Lampard, 42, baada ya kudhibiti mikoba yao kwa kipindi cha miezi 18 pekee.

Nafasi ya Lampard sasa inatarajiwa kutwaliwa na aliyekuwa mkufunzi wa Borussia Dortmund, Thomas Tuchel, aliyetimuliwa na Paris Saint-Germain (PSG) mnamo Disemba 24, 2020.

Kwa mujibu wa gazeti la The Sun nchini Uingereza, Chelsea wamekuwa wakimtafuta kocha anayejivunia umilisi wa lugha ya Kijerumani ili achochee matokeo bora zaidi kutoka kwa Timo Werner na Kai Havertz waliojiunga nao mwanzoni mwa muhula huu kutoka Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).

Lampard ambaye ni kiungo wa zamani wa Chelsea anaondoka uwanjani Stamford Bridge akiwaacha miamba hao waliotawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika nafasi ya tisa kwa alama 29 kwenye msimamo wa jedwali.

Hii ni baada ya Chelsea kupokezwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa Leicester katika mchuano wao uliopita ligini. Awali, kikosi hicho kilikuwa kimesajili ushindi mmoja pekee kwenye jumla ya michuano mitano mfululizo ya EPL.

Mchuano wa mwisho kwa Lampard kusimamia kambini mwa Chelsea ni ule uliowashuhudia masogora wake wakiipepeta Luton Town ya Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Uingereza (Championship) 3-1 kwenye raundi ya nne ya Kombe la FA mnamo Januari 24 ugani Stamford Brigde.

Ushindi huo wa Chelsea ambao walizidiwa maarifa na Arsenal kwa mabao 2-1 kwenye fainali ya Kombe la FA mnamo 2019-20, sasa utawakutanisha na Barnsley kwenye raundi ya tano ya kipute hicho muhula huu.

Lampard aliajiriwa na Chelsea kwa mkataba wa miaka mitatu mnamo Julai 2019 baada ya kuaminiwa kuwa mrithi wa kocha Maurizio Sarri aliyeyoyomea Juventus ambao baadaye walimtimua jijini Turin baada ya msimu mmoja na kumpa mikoba kiungo wao wa zamani, Andrea Pirlo.

Katika msimu wake wa kwanza akidhibiti chombo cha Chelsea, Lampard kikosi hicho kuambulia nafasi ya nne kwenye msimamo wa jedwali la EPL mnamo 2019-20 na kutinga fainali ya Kombe la FA.

Hata hivyo, Chelsea almaarufu The Blues sasa wamepoteza jumla ya mechi tano kati ya nane zilizopita ligini, idadi hiyo ikiwiana na michuano waliyopoteza kutokana na 23 mnamo 2019-20.

Lampard hakusajili mchezaji yeyote katika msimu wake wa kwanza wa ukocha kambini mwa Chelsea kutokana na marufuku iliyochochewa na hatua yao ya kukiuka kanuni za matumizi ya fedha za Uefa.

Hata hivyo, alishawishi kikosi hicho kinachomilikiwa na bwanyenye Roman Abramovich kufungulia mifereji ya fedha katika msimu wake wa pili ambapo Chelsea walitumia zaidi ya Sh30 bilioni kujisuka upya kwa minajili ya kampeni za muhula huu.

Chelsea walijinasia huduma za wanasoka saba wa haiba kubwa wakiwemo Ben Chilwell aliyeagana na Leicester City kwa kima cha Sh6.3 bilioni na Kai Havertz aliyebanduka kambini mwa Bayer Leverkusen ya Ujerumani kwa Sh9.9 bilioni.

Hicho ndicho kiasi kikubwa zaidi cha fedha kwa Chelsea kuwahi kutumia sokoni katika muhula mmoja wa uhamisho wa wachezaji tangu walipojisuka upya kwa juma ya Sh26 bilioni mwanzoni mwa msimu wa 2017-18.

Wanasoka wengine waliosajiliwa na Chelsea mwanzoni mwa msimu huu ni Hakim Ziyech, Xavier Mbuyamba, Malang Sarr, Thiago Silva na Edouard Mendy.

Lampard ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Chelsea, akijivunia mabao 211 kati ya 2001 na 2014. Aidha, anashikilia nafasi ya saba kwenye orodha ya wachezaji waliowahi kuwajibishwa mara nyingi zaidi na timu ya taifa ya Uingereza ambayo aliisakatia mara 106 kwa kipindi cha miaka 15 tangu 1999.

Katika kipindi cha miaka 13 ya usogora uwanjani Stamford Bridge, Lampard alichezeshwa mara 648 na akasaidia Chelsea kutia kibindoni jumla ya mataji 11 yakiwemo manne ya EPL na taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2012.

Kibarua chake cha kwanza cha ukocha kilikuwa kudhibiti mikoba ya Derby County ambao kwa sasa wananolewa na kiungo wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya Uingereza, Wayne Rooney.

Katika msimu wake wa kwanza kambini mwa Derby, Lampard aliongoza kikosi hicho kutinga mchujo wa kupanda ngazi ya kushiriki kivumbi cha EPL ila kikazidiwa maarifa na Aston Villa.

Lampard ndiye kocha wa 10 kuajiriwa kwa mkataba wa kudumu na Abramovich kambini mwa Chelsea tangu mfanyabiashara huyo maarufu mzawa wa Urusi na raia wa Israel kutwaa umiliki wa kikosi hicho mnamo 2003.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, Abramovich ametumia zaidi ya Sh15 bilioni kuwafidia makocha waliowahi kufutwa na Chelsea kabla ya Lampard kupigwa kalamu.

Baada ya kukamilisha kampeni za EPL katika msimu wa 2019-20 kwa alama 66 baada ya kusajili ushindi mara 20 na kupoteza mechi 12, Chelsea kwa sasa wamepoteza michuano sita kutokana na 19 ya ufunguzi wa msimu huu wa 2020-21.

You can share this post!

UDAKU: Neymar hapoi! Sasa amejinasia kidege Emilia wa...

Kingi aungama mambo si shwari kwa ODM Pwani