ODONGO: Kura ya Matungu ni jukwaa kwa Mudavadi kuonyesha umaarufu

Na CECIL ODONGO

UCHAGUZI mdogo wa eneobunge la Matungu ndio utakuwa ratili ya kudhirihisha iwapo Kinara wa ANC Musalia Mudavadi sasa ndiye jogoo wa kisiasa wa jamii ya Mulembe na mwaniaji bora wa Urais kutoka eneo hilo.

Wakati wa mazishi ya mamake katika Kaunti ya Vihiga majuma mawili yaliyopita, viongozi mbalimbali walionekana kurindima ngoma ya Bw Mudavadi na kumsawiri kama kiongozi anayekubalika maeneo yote nchini.

Pia, wengi walifasiri matamshi ya Rais Uhuru Kenyatta kwenye mazishi hayo kuwa Urais haufai kuendea jamii za Kalenjin au Agikuyu kama ishara kuwa alikuwa anamuidhinisha Bw Mudavadi kama mrithi wake 2022.

Hata hivyo, makamu huyo wa Rais lazima amalize vita vya nyumbani na kuwaengua wapinzani wote katika uchaguzi mdogo wa Matungu unaotarajiwa kufanyika mnamo Machi 23 ili kudhihirisha kuwa eneo hilo liko nyuma yake.

Chama cha ANC kilikuwa kikishikilia kiti hicho kupitia marehemu Justus Murunga ambaye tayari alikuwa amehamia kambi ya Naibu Rais Dkt William Ruto kabla ya mauti yake. ANC kimemkabidhi Peter Nabulindo aliyeibuka wa pili katika uchaguzi wa 2017 nafasi ya kupeperusha bendera yake dhidi ya upinzani wa David Were wa ODM na Alex Lanya wa UDA, chama kipya kinachohusishwa na Dkt Ruto.

Kibarua cha kwanza kwa Bw Mudavadi ni kuhakikisha kuwa hakosi udhabiti wa Kaunti ya Kakamega kwa kuwa tayari Gavana Wycliffe Oparanya amekuwa akiendeleza kampeni kali kwa Bw Were ili kuipokonya ANC kiti hicho.

Iwapo, Bw Oparanya atafaulu kuongoza ODM kushinda kiti hicho, basi Bw Mudavadi ataonekana kama kiongozi ambaye hana ushawishi wowote katika eneo la Magharibi ambalo siasa zake zimekuwa zikidhibitiwa na Kinara wa ODM Raila Odinga.

Pili, Bw Mudavadi lazima ajitahidi kuhakikisha kuwa Bw Lanya hapati ushindi kwa kuwa itaonyesha kwamba Naibu Rais ameanza kupenya katika eneo la Magharibi ambapo baadhi ya wabunge wamekuwa wakidai ni ngome ya ANC.

Mara nyingi kinara huyo wa ANC amekashifiwa kwa kutokuwa mkakamavu kusaka kura za nje na kusubiri uungwaji mkono kutoka kwa viongozi maarufu kutoka nje.

Katika uchaguzi wa 2013, Bw Mudavadi alihisi kusalitiwa baada ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto kumwahidi uungwaji mkono kisha kughairi nia hiyo na kuamua kupambana na Bw Odinga debeni.

Vivyo hivyo asichukulie kwa uzito dhana inayoendelea kutamalaki kwamba kwa sasa ana baraka za Rais Kenyatta na yupo katika nafasi bora ya kumrithi mwaka ujao.

Iwapo mwaniaji wake atashinda kule Matungu basi, atakuwa amedhihirisha kuwa anaweza kuwika nyumbani na sasa atakuwa pazuri kusaka uungwaji mkono kutoka maeneo mengine hasa eneo la Kati ambalo kunaonekana kuwa kuna pengo kubwa kisiasa.

Marehemu Masinde Muliro ambaye alikuwa jagina wa kisiasa kutoka eneo la Magharibi wakati wa kupigania mfumo wa vyama vingi 1990, alijizolea umaarufu kutokana na jitihada zake za ukombozi na kupigania maslahi ya raia.

Vivyo hivyo, aliyekuwa Makamu wa Rais marehemu Wamalwa Kijana alidhibiti siasa za Magharibi kabla ya kuaga dunia 2003, kwa kutumia mbinu za kisiasa ambazo zinaoona na matakwa ya raia.

Japo amejikwaa miaka ya nyuma kisiasa hasa 2002 na 2013, Bw Mudavadi anafaa ahakikisha kuwa hakuna mgawanyiko katika ngome yake ambayo ina uwezo wa kumpa kura nyingi zaidi na kumweka kifua mbele dhidi ya wawaniaji wengine wanaomezea mate kiti cha Urais mwakani.

Habari zinazohusiana na hii