• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Tyler Onyango afurahia kuchezeshwa na Ancelotti

Tyler Onyango afurahia kuchezeshwa na Ancelotti

Na GEOFFREY ANENE

MZAWA wa Uingereza mwenye asili ya Kenya, Tyler Onyango ameelezea furaha yake kuchezea timu ya watu wazima ya Everton kwa mara ya kwanza kabisa hapo Januari 24, 2021.

Onyango, ambaye alizaliwa mjini Luton mnamo Machi 4 mwaka 2003, alipewa nafasi hiyo na kocha Mwitaliano Carlo Ancelotti katika mechi ya Kombe la FA ambayo Everton ilichabanga Sheffield Wednesday 3-0 na kuingia raundi ya 16-bora.

Muingereza Dominic Calvert-Lewin, raia wa Brazil Richarlison na raia wa Colombia Yerry Mina walifunga mabao ya Everton katika mchuano huo ambao Ancelotti aliamua kuwapa matineja Onyango, 17, na Thierry Small, 16, nafasi katika dakika 85. Onyango alijaza nafasi ya kiungo mwenzake Andre Gomes, 27, kutoka Ureno naye beki Small akaingia katika nafasi ya kiungo kutoka Colombia James Rodriguez, 29.

Onyango, ambaye Kenya inatumai atakubali kuvalia jezi ya Harambee Stars, alisema baada ya mechi kuwa analenga kutumia fursa hiyo kupiga hatua zaidi katika uchezaji wake uwanjani Goodison Park.

Ameimarika sana katika kipindi cha miezi 12 iliyopita kiasi cha kusukuma Ancelotti kumjumuisha katika timu ya kwanza.

Aliingia katika timu ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 23 msimu uliopita na kujitokeza kuwa mmoja wa wachezaji tegemeo msimu huu katika timu hiyo inayonolewa na David Unsworth.

Onyango amekuwa akifanya mazoezi mara kwa mara na kikosi cha Ancelotti, pamoja na Small, na alikiri kuwa alipokuwa kwenye benchi ya timu ya kwanza alikuwa ameshika roho mkononi.

“Nilijua tukiongoza kwa mabao kadhaa huenda tukapata fursa ya kuonjeshwa mechi hiyo,” alieleza runinga ya evertontv.

“Nilikuwa na wasiwasi, lakini nilipoingia uwanjani nilihisi vizuri na kufurahia.

“Nimekuwa katika klabu hii tangu niwe na umri wa miaka minane, nikajitahidi kupanda katika timu za umri tofauti, na kupata fursa ya kuchezea timu ya kwanza ni kitu kikubwa sana kwangu.

“Ukiwa mtoto, unakuja hapa Goodison, kutazama mechi ama kama watoto wa kuokota mipira (ball boy) na kukaa hapa na kuota tu.

“Ni ndoto, kwa hivyo kuingia uwanjani na kusakata kabumbu ni kitu cha kufurahia sana.

“Kupewa nafasi pamoja na kinda mwingine ambaye pia amepitia katika akademia na kusoma naye, inafanya fursa hiyo kuwa spesheli zaidi.

“Kufanya mazoezi na wachezaji hawa ni kitu cha kujivunia. Katika muda mdogo, unahisi umeimarika sana, makali yako yako juu, kasi ya mchezo wako iko juu, una nguvu za kimwili.”

Onyango alitaja beki wa pembeni kushoto Seamus Coleman, 32, na kiungo wa kati Tom Davies, 22, kuwa wachezaji ambao wamekuwa mchango mkubwa kwake tangu aanze kufanya kazi na kikosi cha watu wazima.

Hakuwa tayari kutaja makocha waliomsaidia katika safari ya kufika aliko sasa akihofia huenda akaacha mmoja nje ya orodha yake.

“Wote wamenisaidia sana kwa njia moja ama nyngine na ninashukuru kila mmoja, kutoka niingie timu ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka minane hadi Under-23,” alisema Onyango.

Aliongeza, “Sikulala nilipofahamu kuwa nimetiwa katika kikosi cha mechi… Ninachostahili kufanya sasa ni kuongeza bidii maradufu ili niweze kupata fursa kama hizi, kuzinyakua na kuridhisha na kufanya niweze kuaminiwa.”

Everton inashikilia nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu kwa alama 32 kutokana na ushindi 10, sare mbili na vichapo vitano.

You can share this post!

KOTH BIRO: Gattuso ashindwa kubeba Ruaraka katika fainali

Serikali yaweka kafyu, operesheni Kapedo