• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Wanasoka 11 waliowahi kunolewa na Sir Alex Ferguson na wakaishia kuwa makocha wakiwemo Rooney na Solskjaer

Wanasoka 11 waliowahi kunolewa na Sir Alex Ferguson na wakaishia kuwa makocha wakiwemo Rooney na Solskjaer

Na CHRIS ADUNGO

WAYNE Rooney, 35, sasa ni kocha wa kikosi cha Derby County nchini Uingereza baada ya kuwa kaimu mkufunzi mkuu wa kikosi hicho tangu Novemba 2020.

Tangu wakati huo, ameongoza kikosi hicho kusajili ushindi mara tatu kutokana na mechi tisa.

Kuteuliwa kwake kuwa kocha mkuu kunamfanya aanze kufuata nyayo za mkufunzi wake Sir Alex Ferguson aliyestaafu rasmi akidhibiti mikoba ya Manchester United mnamo 2013.

Hapa, tunaangazia wachezaji wengine 10 waliowahi kunolewa na Ferguson kisha wakaishia kuwa wakufunzi wa soka.

BRYAN ROBSON

Mnamo 1994, Robson aliteuliwa kuwa kocha wa Middlesbrough kilichomwajibisha pia uwanjani kama mchezaji katika baadhi ya mechi.

Miaka mitatu baadaye, aliangika daluga zake ili kujitosa kabisa katika ulingo wa ukufunzi.

Aliongoza Middlesbrough kupanda ngazi hadi Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 1995 na akasajili wanasoka matata akiwemo Fabrizio Ravanelli.

Hata hivyo, hakusaidia kikosi chake kutwaa taji lolote baada ya kupoteza nusu-fainali mbili – moja dhidi ya Leicester City kwenye Coca-Cola Cup na nyingine dhidi ya Chelsea kwenye Kombe la FA.

Baada ya kupigwa kalamu mnamo 2001, Robson alipokezwa mikoba ya Bradford kabla ya kuwa kocha wa West Bromwich Albion, Sheffield United na timu ya taifa ya Thailand. Robson hajawahi kuwa kocha wa timu yoyote tangu 2011.

STEVE BRUCE

Tangu 1998, nahodha huyu wa zamani wa Man-United ameteuliwa kuwa kocha mara 11 (mara mbili kambini mwa Wigan Athletic).

Alihudumu kwa muda mrefu zaidi kambini mwa Birmingham City aliowaongoza kupanda ngazi hadi EPL mnamo 2007.

Bruce ambaye kwa sasa anawatia makali masogora wa Newcastle United, aliwahi pia kuwanoa Hull City mnamo 2013 na akawaongoza kutinga fainali ya Kombe la FA ambapo walizidiwa maarifa na Arsenal uwanjani Wembley.

ROY KEANE

Keane alianza vyema kazi ya ukocha kwa kuwaongoza Sunderland kupanda ngazi kutoka Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship) hadi EPL mnamo 2007.

Hata hivyo, safari yake katika ulingo huo ilikabiliwa na pandashuka tele katika msimu uliofuata baada ya waajiri wake kupokezwa kichapo kimono cha 7-1 kutoka kwa Everton kwenye mechi ya EPL ugani Goodison Park.

Baada ya Sunderland kusajili matokeo duni katika msimu wa 2018-19, Keane aliagana na kikosi hicho baada ya uhusiano kati yake na mmiliki wa zamani wa kikosi hicho Ellis Short na aliyekuwa mwenyekiti Niall Quinn kusambaratika.

Keane aliwahi pia kupokezwa mikoba ya kikosi cha Ipswich Town kilichomfuta kazi mnamo 2011 kwa sababu ya matokeo duni.

OLE GUNNAR SOLSKJAER

Sogora huyo wa zamani wa Man-United aliwaongoza Molde kutwaa taji la Ligi Kuu ya Norway chini ya ukufunzi wake kati ya 2011 na 2014.

Hata hivyo, nyota yake katika ulingo huo wa ukufunzi haikung’aa jinsi ilivyotarajiwa baada ya kupokezwa mikoba ya Cardiff City mnamo 2014.

Cardiff waliteremshwa ngazi baada ya kuvuta mkia kwenye jedwali la EPL na Solskjaer akafutwa kazi miezi tisa baada ya uteuzi.

Aliaminiwa fursa ya kuwa mrithi wa kocha Jose Mourinho ugani Old Trafford mnamo 2018 na amechangia ufufuo mkubwa wa Man-United katika soka ya EPL.

MARK HUGHES

Alianza kazi ya ukocha akidhibiti mikoba ya timu ya taifa ya Wales kati ya 1999 na 2004. Nusura awaongoze Wales kufuzu kwa fainali za Euro 2004 kabla ya masogora wake kuzidiwa ujanja na Urusi kwenye mchujo.

Aliyoyomea baada ya katika klabu ya Blackburn na akawasaidia kusalia kwenye kampeni za EPL na kufuzu kwa nusu-fainali za Kombe la FA mnamo 2005.

Katika msimu uliofuata, aliwaongoza Blackburn kukamilisha kampeni za EPL ndani ya mduara wa sita-bora. Matokeo hayo mazuri yalimpa sifa na akaajiriwa na Manchester City waliompiga kalamu mwaka mmoja baadaye.

Alipokezwa mikoba ya Fulham baadaye kabla ya kusajili matokeo duni kambini mwa Queens Park Rangers (QPR).

Hughes alihudumu kambini mwa Stoke City kwa miaka mitano kabla ya kutimuliwa na kikosi hicho mnamo 2018. Ni katika mwaka uo huo ambapo alipigwa kalamu na Southampton pia baada ya michuano 27 pekee.

PAUL INCE

Nyota yake katika ulingo wa ukocha ilianza kung’aa akidhibiti mikoba ya MK Dons mnamo 2007-08 na akawaongoza kutwaa taji la Football League Trophy baada ya kufunga Grimsby 2-0.

Baadaye, aliwaongoza waajiri wake kupanda ngazi hadi Ligi ya Daraja la Pili katika soka ya Uingereza. Hatua hiyo iliwafanya Blackburn Rovers kuwa kikosi cha kwanza kuajiri kocha mwenye asili ya Kiafrika katika Ligi Kuu ya EPL.

Hata hivyo, alifutwa kazi kabla ya Krismasi baada ya kuongoza waajiri wake kushinda mechi tatu pekee kati ya 17.

Alirejea MK Dons ila akashindwa kuendeleza rekodi nzuri aliyojivunia awali. Alijiunga baadaye na Notts County ambapo alishuhudia kikosi chake kikipoteza mechi tisa mfululizo na akafurushwa na kikosi cha Blackpool baada ya msimu mmoja pekee mnamo 2014.

GARY NEVILLE

Nyota huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa Valencia mnamo 2015 huku akisaidiwa na kakaye Phil Neville.

Hata hivyo, Valencia walishindwa kufuzu kwa raundi ya pili ya mchujo wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) ambapo walipokezwa kichapo cha 7-0 kutoka kwa Barcelona na wakapiga jumla ya mechi tisa mfululizo bila ushindi.

Katika mchuano wa Europa League uliowakutanisha na Athletic Bilbao, Neville alionyeshwa kadi nyekundu kwa kulalamikia uhalali wa bao la wapinzani na kikosi chake kikaaga mashindano hayo hatimaye.

Neville alitimuliwa baada ya kusimamia Sevilla katika mechi 16 pekee za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga). Wakati wa kufutwa kwake, kikosi chake kilikuwa kimeshinda mechi tatu pekee na kushuka hadi nafasi ya 14 jedwalini.

PHIL NEVILLE

Alianza safari yake ya ukufunzi akishikilia mikoba ya Salford City mnamo 2015.

Hata hivyo, ni katika soka ya wanawake ambapo ukubwa wa uwezo wake wa ukufunzi umedhihirika hadi kufikia sasa.

Neville tayari ameagana na timu ya taifa ya soka ya wanawake nchini Uingereza na ametua kambini mwa Inter Miami inayomilikiwa na mwanasoka David Beckham aliyewahi kuchezea Man-United na Real Madrid.

Maamuzi yake ya kuagana na timu ya taifa ya Uingereza yalifikiwa mnamo Agosti 2020 baada ya vipusa wake kupoteza mechi saba kati ya 11, hii ikiwa rekodi mbovu zaidi kuwahi kusajiliwa na kikosi hicho tangu 2003.

RYAN GIGGS

Mnamo 2014, Giggs aliteuliwa kuwa kocha mshikilizi wa Man-United baada ya kutimuliwa kwa mkufunzi David Moyes.

Alisimamia michuano minne ya mwisho wa msimu ambapo aliongoza kikosi chake kushinda mbili, kuambulia sare mara moja na kupoteza nyingine moja kabla ya ujio wa mkufunzi Louis van Gaal aliyetwaa mikoba na Giggs kufanywa msaidizi wake.

Mnamo 2018, Giggs alipokezwa ukocha wa timu ya taifa ya Wales baada ya kuaminiwa kujaza nafasi ya Chris Coleman na akaongoza Wales kufuzu kwa fainali za Euro 2020.

Wales walipanda ngazi baadaye kwenye UEFA Nations League hadi Kundi la League A baada ya kuongoza Kundi 4 League B kwenye kampei za 2020-21.

Hata hivyo, ni msaidizi wake Rob Page aliyesimamia michuano miwili ya mwisho katika hatua ya makundi baada ya Giggs kushauriwa kujiondoa kwa muda kutokana na kisa ambapo alitiwa nguvuni kwa kumjeruhi mchumba wake, Kate Greville.

LAURENT BLANC

Hakuna mchezaji yeyote mwingine ambaye amewahi kucheza chini ya Sir Alex Ferguson na akajivunia ufanisi wa kujitwalia idadi kubwa ya mataji akiwa kocha kuliko Blanc.

Mshindi huyo wa Kombe la Dunia aliwaongoza Bordeaux kutwaa mataji mawili katika soka ya Ufaransa mnamo 2009 kabla ya kuongoza PSG wakinyanyua mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) kati ya 2013-16 na mengine mawili ya makombe tofauti.

Blanc aliwahi pia kuwa kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa na akajiuzulu baada ya miaka miwili kufuatia kichapo cha 2-0 ambacho Ufaransa walipokezwa na Uhispania kwenye robo-fainali za Euro 2012.

Baada ya kuwa nje kwa muda mrefu bila kikosi cha kunoa, Blanc aliajiriwa na kikosi cha Al-Rayyan nchini Qatari mnamo Disemba 2020.

You can share this post!

Everton wazamisha chombo cha Sheffield Wednesday kwenye...

Kasisi aponda Uhuru