• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Leicester wakomoa Brentford na kujikatika tiketi ya kuvaana na Brighton kwenye raundi ya tano ya Kombe la FA

Leicester wakomoa Brentford na kujikatika tiketi ya kuvaana na Brighton kwenye raundi ya tano ya Kombe la FA

Na MASHIRIKA

LEICESTER City walitoka nyuma na kuzamisha chombo cha Brentford kwa mabao 3-1 katika mchuano wa raundi ya nne ya Kombe la FA mnamo Jumapili.

Brentford waliokuwa wakichezea nyumbani kwao walichukuwa uongozi wa mapema kupitia bao la Mads Bech Sorensen katika dakika ya sita.

Ingawa hivyo, Leicester wanaotiwa makali na kocha Brendan Rodgers walirejea ugani kwa minajili ya kipindi cha pili kwa matao ya juu na wakasawazishiwa na Cengiz Under chini ya sekunde 50 za mwanzo wa kipindi cha pili kupitia krosi ya kiungo James Maddison.

Dakika tano baadaye, Youri Tielemans alifungia Leicester bao la pili kupitia mkwaju wa penalti kabla ya Maddison kukamilisha karamu ya mabao katika dakika ya 71.

Matokeo hayo yalirejesha kumbukumbu za msimu uliopita wa 2019-20 ambapo Leicester ambao kwa sasa watavaana na Brighton kwenye raundi ya tano, walipepeta Brentford 3-1 katika raundi ya nne ya Kombe la FA.

Brentford hawajawahi kushinda mechi yoyote dhidi ya Leicester katika jumla ya mechi saba zilizopita katika kivumbi cha kuwania Kombe la FA na hawajawahi kuwazidi maarifa katika pambano lolote tangu 1953.

Hata hivyo, Brentford walijituma vilivyo katika tukio lililopania kudhihirisha kwamba walistahili kupepeta vikosi vinne vya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu na kufuzu kwa nusu-fainali za Carabao Cup ambapo walibanduliwa mwishowe na Tottenham Hotspur ya kocha Jose Mourinho.

Mechi kati ya Brenford na Leicester ilileta pamoja kikosi kinachoshikilia kwa sasa nafasi ya nne kwenye jedwali la Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Uingereza (Championship) na kingine kinachoshikilia nafasi ya tatu kwenye jedwali la EPL.

Kocha Rodgers kwa sasa ametinga raundi ya tano ya Kombe la FA mara nne – mara mbili akidhibiti mikoba ya Liverpool na mara mbili akiwanoa masogora wa Leicester.

Kwa upande wao, Brentford wamebanduliwa nje ya Kombe la FA mara 13 kati ya 14 zilizopita dhidi ya vikosi vya EPL. Mara ya pekee walipokosa kushuhudia tukio hilo ni mnamo Januari 2006 walipowacharaza Sunderland 2-1.

Ni mara ya kwanza tangu Novemba 2008 kwa Leicester kufunga mabao matatu na zaidi kwenye michuano miwili mfululizo ya Kombe la FA.

Maddison amehusika moja kwa moja katika mabao 13 ambayo yamefungwa na Leicester katika mechi 24 zilizopita msimu huu wa 2020-21. Nyota huyo raia wa Uingereza amefunga mabao tisa na kuchangia mengine manne. Katika msimu wa 2019-20, kiungo huyo alihusika katika mabao 12 pekee ya waajiri wake kutokana na jumla ya michuano 38.

You can share this post!

Bayern waponda Schalke na kufungua mwanya wa alama saba...

Barcelona wacharaza Elche na kupaa hadi nafasi ya tatu...