• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Barcelona wacharaza Elche na kupaa hadi nafasi ya tatu kwenye jedwali la La Liga

Barcelona wacharaza Elche na kupaa hadi nafasi ya tatu kwenye jedwali la La Liga

Na MASHIRIKA

KIUNGO mkabaji wa Barcelona, Frenkie de Jong alifunga bao na kuchangia jingine katika ushindi wa 2-0 uliosajiliwa na waajiri wake dhidi ya Elche katika mechi ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Jumapili.

De Jong alichuma nafuu kutokana na masihara ya beki Diego Gonzalez wa Elche na kuwaweka Barcelona kifua mbele kunako dakika ya 39.

Nyota huyo raia wa Uholanzi alichangia bao la pili la Barcelona lililofungwa na Riqui Puig aliyecheka na nyavu za wapinzani kwa mara ya kwanza akivalia jezi za Barcelona waliokuwa wakimwajibisha katika mechi yake ya 25.

Elche nusura wasawazishe mambo mwanzoni mwa kipindi cha pili ila kombora la fowadi Emiliano Rigoni likadhibitiwa vilivyo na kipa Marc-Andre ter Stegen.

Juhudi za Barcelona pia kufunga mabao zaidi katika kipindi cha pili zilizimwa na kipa Edgar Badia wa Elche ambaye aliwanyima wachezaji Ousmane Dembele na Francisco Trincao nafasi za wazi.

Mechi hiyo ilikuwa ya 13 mfululizo kwa Elche kupiga bila ya kusajili ushindi. Matokeo hayo kwa sasa yanawaweka katika hatari ya kuteremshwa ngazi mwishoni mwa kampeni za msimu huu ikizingatiwa kwamba wanashikilia nafasi ya 19 kwa alama 17, nne pekee kuliko Huesca wanaovuta mkia.

Hata hivyo, wangali na mechi mbili zaidi za kusakata ili kufikia idadi ya michuano 20 ambayo tayari imetandazwa na Alaves, Osasuna, Real Valladolid na Eibar waliopo juu yao.

Chini ya kocha Ronald Koeman, Barcelona walichupa hadi nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 37, tatu nyuma ya nambari mbili Real Madrid.

You can share this post!

Leicester wakomoa Brentford na kujikatika tiketi ya kuvaana...

Wanyakuzi wa ardhi iliyotengewa barabara za kutumiwa...