• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
Wanyakuzi wa ardhi iliyotengewa barabara za kutumiwa mitaani wakati wa dharura waonywa

Wanyakuzi wa ardhi iliyotengewa barabara za kutumiwa mitaani wakati wa dharura waonywa

Na SAMMY KIMATU

MSIMAMIZI mmoja katika Kaunti ya Nairobi ameonya wamiliki wa nyumba walionyakua barabara mitaani na kujenga nyumba kwamba wanahatarisha maisha ya watu.

Akiongea na Taifa Leo mnamo Jumatatu, Msaidizi wa Kamishna wa kaunti wa eneo la South B, Bw Michael Aswani Were alisema wahusika hawana mioyo ya utu na badala yake wamejawa na famaa ya pesa.

Aidha, Bw Were ameagiza kila mmiliki wa nyumba kuhakikisha ametenga nafasi ya wakazi ili wawe wakitumia wakati wa dharura akitoa mfano wa visa vya moto hasa mitaani ya mambanda.

“Kuna baadhi ya wamiliki wa nyumba walionyakua njia zilizotengwa kwa minajili ya kutumia wakati wa dharura kama vile mikasa ya moto na pia ambulensi zikija kuchukua wagonjwa au magari ya polisi wanapokuwa kazini,” Bw Were aliongea hayo baada ya kukagua eneo la kisa cha moto katika mtaa wa Sokomoko karibu na Kituo cha Biashara cha South B wiki moja iliyopita.

Kwa mujibu wa ripoti ya kamati ya usalama katika tarafa, hakukuwa na njia ya kutumiwa wakati wa dharura ndiposa moto uliteketeza nyumba nyingi.

Wamiliki wa nyumba hizo, waliolaumiwa kwa tamaa ya pesa walinyajua ardhi yote na kujenga nyumba.

“Wamiliki wa mtaa huu ni watu wasiokuwa na ubinadamu kwa kutowacha barabara za magari. Ilikuwa ni vingumu kwa gari za kuzima moto kuingia kwenye eneo mkasa kuzima moto. Kungekuwa na njia, tusingepata nyumba nyingi kuteketea siku hiyo,’’ Bw Were akasema.

Baada ya tukio hilo, alionya pia watu wasiruhusiwe kujenga nyumba za orofa za mabati kwani hilo nalo linachangia pakubwa hasara kupatikana zaidi wakati wa moto.

Aliongeza kwamba kwa miujibu wa ripoti za majasusi, mitaa ilikuwa na barabara hapo awali. Hata hivyo, leo kuna msongamano wa nyumba baada ya wanyakuzi wa ardhi kunyakua nafasi zote mitaani, “Nimefahamishwa kulikuwa na barabara zilizokatwa mitaani na watangulizi wangu wakishirikiana na machifu. Lazima baranbara zipatikane mitaani yetu,” Bw Were akaongeza.

Tarafa ya South B ina msururu wa mitaa ya mabanda zaidi ya kumi ma visa vya moto kwenye mitaa hiyo sio jambo geni kutokana na idadi kubwa ya watu, miundo misingi mbovu na pia nyumba nyingi ni za mabati.

Wakazi kwenye mitaa hiyo ni wa daraja la chini ikizingatiwa kuna ukosefu wa ajira miongongi mwa wengi wao. Badhi ya ni vibarua katika eneo la viwanda huku wamama wakifanya kazi za sulubu mitaani mingine kwa kufua nguo.

  • Tags

You can share this post!

Barcelona wacharaza Elche na kupaa hadi nafasi ya tatu...

LISHE NA VINYWAJI: Manufaa ya juisi