• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:05 AM
KCB kufufua uhasama wao na Kabras RFC kwenye raga ya Charity Cup

KCB kufufua uhasama wao na Kabras RFC kwenye raga ya Charity Cup

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Kenya Cup, KCB, watashuka dimbani kuvaana na washikilizi wa Enterprise Cup, Kabras RFC, kuwania taji la Charity Cup mnamo Februari 20.

Kivumbi hicho kitapigwa wiki moja kabla ya kampeni za Ligi Kuu ya Raga kwa minajili ya msimu huu kuanza rasmi.

KCB na Kabras ndizo klabu mbili ambazo zimekuwa zikitamalaki kampeni za raga ya Kenya kwa kipindi cha misimu mitano iliyopita.

Kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa ligi kupulizwa rasmi mnamo Februari 27, vikosi sita vya ligi ya chini (KRU Championship) vitapigania nafasi mbili za kupanda ngazi kushiriki Kenya Cup katika juhudi za kujaza nafasi za Western Bulls na Kisumu RFC walioteremshwa ngazi muhula uliopita wa 2019-20. Michuano hiyo ya mchujo itapigwa mnamo Februari 6 na 13.

Kabras walisajili ushindi wao wa kwanza dhidi ya KCB mnamo Novemba 2019 walipowapiga wanabenki hao 19-6 uwanjani Ruaraka baada ya kuambulia pakavu kwenye majaribio 10 ya awali.

Miamba hao wawili wa raga ya Kenya wamewahi kukutana mara nne kwenye fainali za Kenya Cup huku KCB wakiibuka washindi katika makala yote hayo. KCB waliwashinda Kabras 27-3 mnamo 2015 uwanjani RFUEA, 36-8 mnamo 2017 ugani Lions Den Ruaraka, 29-24 mnamo 2018 (Ruaraka) na 23-15 mnamo 2019 mjini Kakamega.

Kabras walitia kapuni taji lao la kwanza na la pekee kwenye kampeni za Kenya Cup mnamo 2016 baada ya kuwacharaza Impala Saracens 22-5 uwanjani Impala Club.

“Mechi dhidi ya Kabras itakuwa kipimo halisi cha maandalizi yetu kwa minajili ya kibarua cha msimu huu. Ni mchuano utakaotuchorea picha kamili ya kikosi na kutuonyesha mahali tulipo. Mechi hiyo itatufichulia udhaifu wetu na kutupa jukwaa zuri la kujirekebisha mapema na kufahamu tunachotarajia ligini muhula huu,” akatanguliza mwenyekiti wa KCB, Xavier Makuba.

“Msimu utakuwa mgumu kwa kila mshindani kwa sababu hakuna kikosi kimepata fursa ya kujiandaa vya kutosha,” akaongeza kinara huyo.

Kwa upande wake, Philip Jalang’o ambaye ni mwenyekiti wa Kabras amesema kikosi chake kinapania kuimarisha kiwango cha mazoezi katika kipindi cha wiki nne zijazo ili kujiweka sawa kwa kampeni za msimu huu ligini.

Mechi za ligi zitakuwa za mkondo mmoja pekee msimu huu na zitachezwa kwa kipindi cha wiki 11 ambapo vikosi vinne vya kwanza vitafuzu kwa nusu-fainali ambazo zimeratibiwa kupigwa Mei 22 kabla ya fainali kufuata wiki moja baadaye.

Katika siku ya kwanza ya msimu huu, Impala watavaana na Kenya Harlequins, Homeboyz wapepetana na Nondies nao Mwamba washuke ugani kukwaruzana na Blak Blad. Oilers watakuwa wenyeji wa Nakuru RFC.

You can share this post!

Olunga afunga hat-trick akisaidia Al Duhail kukung’uta Al...

Wasiwasi huku vituo vya damu vikikauka