WASONGA: Ruto, Raila wasaidie kutatua shida za Kenya si kulumbana

Na CHARLES WASONGA

MALUMBANO yanayoendelea kati ya Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga kuhusu nani anapasa kulaumiwa kuhusu kufeli kwa Jubilee katika utendakazi wake, hayana manufaa yoyote wakati ambapo taifa linakumbwa na changamoto nyingi.

Ni unafiki mkubwa kwa Dkt Ruto kudai kuwa Bw Odinga ndiye alivuruga Jubileee alipofanya maridhiano ya kisiasa na bosi wake Rais Uhuru Kenyatta.

Hii ni kwa sababu Rais Kenyatta mwenyewe amewahi kuwafichulia Wakenya kwamba alimshirikisha Dkt Ruto katika hatua zote za mwafaka huo hadi kuasisiwa kwa mpango wa maridhiano (BBI).

Kwa hivyo malumbano hayo yanadhihirisha kuwa wanasiasa hawa wawili hawajali maslahi ya Wakenya na kwamba kinachowaongoza ni tamaa ya kuingia Ikulu mwaka ujao.

Kwa mfano, ni jambo la kuudhi kwamba Dkt Ruto anatumia muda mwingi na rasilimali za umma kuongoza mikutano katika makazi yake ya Karen, Nairobi, kujadili mikakati ya kampeni za urais ilhali majangili wanavuruga maisha ya wakazi katika eneo la Kapedo.

Kama msaidizi wa Rais katika utekelezaji wa majukumu yake, alivyodai juzi akiwa Embu, Dkt Ruto alifaa kuzuru eneo hilo kujaribu kupatanisha pande hasimu.

Kufikia sasa jumla ya watu 10 wameuawa katika eneo hilo la mpaka wa kaunti za Baringo na Turkana. Inasikitisha kuwa wanne kati ya waliouawa ni maafisa wa polisi.

Dkt Ruto ambaye anatoka jamii ya wafugaji hajatoa taarifa yoyote kulaani mauaji yanayoendelea Kapedo au mapigano ya kikabila yanayoendelea katika Kaunti ya Marsabit.

Juzi alipokutana na madiwani kutoka Kaunti ya Mandera katika makazi yake ya Karen, taarifa kutoka kitengo chake cha mawasiliano ilisema kuwa Naibu Rais aliitisha mkutano huo kujadili mapigano ya kikabila katika Kaunti ya Mandera na eneo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya kwa ujumla.

Lakini baadaye ilibainika kuwa miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa katika mkutano huo ni mchakato wa BBI na azma yake ya kuingia Ikulu 2022.

Hii ni kielelezo cha kufeli kwa serikali ya Jubilee katika kutekeleza wajibu wake wa kikatiba wa kulinda maisha na mali ya wananchi. Kufeli huko pia kunathibitishwa na kimya cha Rais Kenyatta ilhali yeye ndiye kamanda mkuu wa walinda usalama wanaoangamizwa Kapedo.

Bw Odinga pia amefeli kwa kutotoa taarifa zozote kuhusu visa vya utovu wa usalama katika maeneo hayo ilhali ni mwanasiasa anayemezea mate kiti cha urais mwaka ujao.

Tuliona juzi akitoa taarifa kuhusu mgomo wa wahudumu wa afya na mvutano kati ya Tume ya Huduma za Walimu (TSC) na Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT).

Habari zinazohusiana na hii