TAHARIRI: Tuhimize maadili kwa watoto wetu

KITENGO CHA UHARIRI

TANGU shule zifunguliwe upya kwa muhula wa pili mwanzoni mwa mwezi huu, tumekuwa tukisikia matukio yanayoonyesha utovu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi.

Awali wanafunzi walienda shuleni wakiwa na silaha na kuwashambulia walimu wao. Kisha tukasikia visa vya wanafunzi wadogo kujihusisha na mapenzi, huku wengine wakijaribu kuwaua wazazi wao kwa kukanywa kuhusu tabia kama hizo.

Sasa hivi jambo linaloonekana kuwa mtindo kwa wanafunzi wa shule za bweni ni kuchoma mabweni hayo.

Vitendo hivi kwa kiasi fulani vimechangiwa na watoto kukaa nyumbani kwa muda mrefu. Wataalamu wa saikojolia watathibitisha kwamba, kwa kukaa nyumbani karibu miezi kumi, kumefanya baadhi ya wanafunzi kujihusisha na shughuli za kijamii. Wengi walikuwa waendeshaji bodaboda maarufu, wengine labda hata walijihusisha na mahusiano ambapo wanajichukulia kuwa baba au mama wa familia.

Kwa kujichukulia kuwa watu wazima, wengine huonyesha upinzani kwa mtu yeyote anayejaribu kuwadhibiti.

Lakini pia likizo ilionyesha upungufu uliopo miongoni mwa baadhi ya wazazi kuhusu mbinu bora za kuwalea watoto. Kubwa zaidi ni kukosekana kwa mafunzo ya kiroho, ambayo hutekeleza wajibu mkubwa katika kuweka msingi bora wa maisha ya watoto.

Kwa hivyo kurejelea mafunzo ya kidini kwa watoto katika madrasa na makanisa ni jambo la maana ambalo kila mzazi apaswa kulikubali na kuunga mkono.

Baraza la Viongozi wa dini mbalimbali lililobuniwa kudhibiti idadi ya wanaofika makanisani na misikitini, lilitangaza kwamba sasa watoto wadogo pia wanaweza kuhudhuria mafunzo ya madrasa na yale yanayotolewa makanisani, maarufu kama ‘Sunday School’.

Mafunzo hayo yanahitajika zaidi wakati huu, ambapo hata watoto wadogo wameingizwa kwenye janga la kutumia simu. Kwa kukosa mbinu za kuwatuliza watoto wao, wazazi wengi wamewaachia watoto wao simu wachezee. Lakinisimu hizo zikiwa na mtandao wa intaneti, zina mambo mengi yanayoweza kuathiri maadili, tabia na mitazamo ya watoto.

Kwa kuwa walimu wengi wa taasisi hizo za kidini hawana mishahara ya kueleweka, ipo haja kwa mashirika ya kijamii na hata serikali kuwatengea kiasi kidogo cha pesa kama mshahara.

Habari zinazohusiana na hii