• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 5:55 AM
VITUKO: Pengo alaghaiwa na mwanafunzi mjanja kuvunja amri ya mkuu kutowapa watoto simu

VITUKO: Pengo alaghaiwa na mwanafunzi mjanja kuvunja amri ya mkuu kutowapa watoto simu

Na SAMUEL SHIUNDU

JUA la Januari liliwahujumu wanajamii bila ubaguzi.

Shuleni, hali hii hudhihirishwa na kiherehere cha wanafunzi kuwaomba walimu simu ili wakawasiliane na wazazi. Hali haikuwa tofauti kwa wanafunzi wa shuleni Sidindi.

Tangu mwalimu mkuu wa Sidindi awajuze walimu hatari ya kuwapa simu wanafunzi, Pengo aliamua kutahadhari kabla ya hatari. Hakutaka kujiingiza kwenye tatizo hususa wakati huo ambao shule nyingi zilikuwa zinashuhudia migomo ya wanafunzi.

“Ongea na mwalimu wako wa darasa,” ndivyo alivyomwambia kila aliyekuja kumwomba simu.

Lakini wanafunzi wa Pengo walikuwa werevu kuliko alivyowachukulia. Walifahamu kuwa aliwapenda wenye nidhamu na wenye mazoea ya kushauriana na walimu.

Mmoja wa wanafunzi walioijua siri hii ni Kalulu. Huyu alimjia Pengo na maswali mengi ya kimasomo kama chambo cha kujenga mlahaka mwema na mwalimu Pengo. Alimuuliza hili na lile na hatimaye akalifikie lile haswa lililompeleka afisini, “Mwalimu nisaidie simu nikawasiliane na mzazi wangu.”

Pengo aliwaza na kuwazua la kufanya. Ni kana kwamba mwanafunzi huyo alikuwa amemweka kwenye kishawishi ambacho wakristu huomba kuepushiwa. Kumpa simu kungehatarisha taaluma yake na kumnyima kungemvunja moyo mwanafunzi huyu mwema aliyekuwa katambua umuhimu wa kushauriana na walimu. Hatimaye akapiga moyo konde na kumpa mwanafunzi huyo simu lakini kwa masharti.

Mwanzo, Kalulu alikumbushwa kutumia Kiswahili. “Ndiyo mwalimu,” mwanafunzi alimjibu mwalimu wake kwa unyenyekevu. Pia, alipaswa kuwasiliana na mzazi wake kwa kutumia ujumbe mfupi na wala si kupiga simu.

Tatu na muhimu pia ni kuwa Kalulu alipaswa kumsisitizia mzazi kutuma pesa yoyote ambayo angetuma kwa simu ya mwalimu wa darasa.

“Hakikisha umemsisitizia kutuma pesa zozote unazohitaji kwa mwalimu wako wa darasa!” Pengo alikumbusha kwa mara ya ngapi sijui.

Kalulu aliyafwata masharti kwa sababu alikuwa mhitaji na mhitaji ni mtumwa daima. Akawasiliana na mzazi wake kwa ujumbe na kurejea darasani. Pengo alipoitwaa simu yake, akapitia jumbe za huyo mwanafunzi tena ili kuhakikisha kuwa mwanafunzi hajasema lolote ambalo linaweza kuleta tatizo.

Ujumbe mmojawapo ulimchanganya Pengo akashindwa jinsi ya kuuchukulia. Kwenye ujumbe huu, mwanafunzi alimsisitizia mzazi wake kutumia nambari ya mwalimu wa darasa kutuma pesa.

“Mwenye simu hii pia ni mwalimu wetu ila simwamini na tena ni kama amefuliza,” mwanafunzi alikuwa kamjuza mzazi wake.

You can share this post!

Afisa wa polisi auawa na majambazi eneo la Land Mawe

Maafisa wa DCI wamkamata mwanamume anayeshukiwa kumuua...