• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Chipu kutetea Kombe la Afrika mwezi Machi, ratiba ya Shujaa, Lionesses na Simbas pia imetangazwa

Chipu kutetea Kombe la Afrika mwezi Machi, ratiba ya Shujaa, Lionesses na Simbas pia imetangazwa

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Raga barani Afrika (Rugby Africa) limetangaza tarehe za Kombe la Afrika la chipukizi 2021 (Barthes Trophy) ambalo Kenya sasa itaandaa Machi 25 hadi Aprili 4 jijini Nairobi.

Wenyeji Kenya, ambao timu yao ya chipukizi inafahamika kama Chipu, watakuwa wakitetea taji lao dhidi ya Namibia, Senegal na Madagascar. Mshindi atajikatia tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia la daraja la pili almaarufu Junior World Rugby Trophy (JWRT) mwezi Septemba.

Chipu waliduwaza mabingwa wa miaka nyingi Namibia 21-18 katika fainali ya Barthes Trophy katika klabu ya michezo ya KCB mtaani Ruaraka mwezi Aprili 2019 na kushiriki JWRT nchini Brazil.

Walifaa kutetea taji lao la Barthes Trophy mnamo Aprili 2020, lakini mkurupuko wa virusi hatari vya corona ulifanya dimba hilo pamoja na mashindano mengine yote ya Rugby Africa kuahirishwa.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari Januari 25, shirikisho hilo lilitangaza pia litaandaa Kombe la Afrika la wachezaji 15 kila upande la wanaume na pia wanawake. Pia, Kombe la Afrika la wachezaji saba kila upande la wanaume liko kwenye ratiba pamoja na lile la wanawake.

“Huku raundi ya kwanza ya mashindano hayo yote ikianza Machi, timu tayari zimezamia mazoezi. Kwa mujibu wa mataifa wanachama na wachezaji, kila mtu anasubiri kwa hamu kubwa kushiriki mechi,” alisema Naibu Rais wa Rugby Africa, Andrew Owor.

Mganda huyo aliongeza kuwa wanafahamu kuwa kuwepo kwa janga la corona bado kunaweza kusababisha kuahirishwa ama kufutiliwa mbali kwa mashindano hayo kwa ghafla.

Iwapo Barthes Trophy itaahirishwa kutoka tarehe zilizopendekezwa, Owor amesema linaweza kufanyika mwezi Juni. Shindano hilo la wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 litaleta pamoja timu nne-bora ambazo ni Kenya, Namibia, Senegal na Madagascar.

Mwezi Mei utakuwa zamu ya timu za Botswana, Burkina Faso, Burundi, Cameroon, Eswatini, Mauritius, Morocco, Nigeria na Rwanda kupigania tiketi ya kuingia mechi za makundi za Kombe la Afrika la wanaume. Lisipofanyika mwezi huo, limetengewa mwezi wa Julai.

Mechi za makundi za dimba hilo zitang’oa nanga Julai, huku makundi manne ya timu tatu yakipangwa. Kila kundi litachezewa katika eneo tofauti.

Timu zitakazokamilisha makundi hayo katika nafasi mbili za kwanza, zitaingia Kombe la Afrika 2022 ambalo litatumiwa kuchagua mwakilisha wa Bara Afrika katika Kombe la Dunia 2023. Kombe la Afrika la wanawake pia litafanyika wakati huo.

“Mwaka 2021, Namibia, Kenya, Uganda na Tunisia huenda wakapata haki za kuwa wenyeji, lakini tuzo kubwa litaendea timu zitakazoshinda ambazo zitashiriki mashindano makubwa ya mwaka 2022,” alitabiri afisa anayesimamia raga ya wanawake katika shirikisho hilo Maha Zaoui.

Mwezi wa Novemba umetengwa kuandaa Kombe la Afrika la wanaume na pia lile la wanawake la raga ya wachezaji 15 kila upande ikiwa hayatafanyika katika kipindi cha kwanza.

Makombe ya raga ya wachezaji saba kila upande yataanza na mchujo mwezi Agosti na Septemba yakitangulizwa na mashindano ya maeneo manne. Yote yatafanyika katika eneo moja.

Miezi ya Oktoba, Novemba na Desemba imetengwa kuandaa mashindano yatakayokuwa yameahirishwa kwa sababu ya janga la corona. 

  • Tags

You can share this post!

Kalonzo, Muthama, Mutua kupimana ubabe kampeni zikianza kwa...

NGILA: Nchi za Afrika zikumbatie teknolojia kama Kenya