• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:45 AM
Kamworor na Obiri watiwa kwenye orodha ya wanariadha watakaotifua kivumbi cha Ras Al Khaimah Nusu Marathon mnamo Februari 19

Kamworor na Obiri watiwa kwenye orodha ya wanariadha watakaotifua kivumbi cha Ras Al Khaimah Nusu Marathon mnamo Februari 19

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa zamani wa dunia katika mbio za nusu marathon, Geoffrey Kamworor na bingwa wa dunia katika mbio za mita 5,000, Hellen Obiri, wamejumuishwa kwenye orodha ya wanariadha watakaonogesha kivumbi cha kilomita 21 cha Ras Al Khaimah (RAK Half Marathon) mnamo Februari 19, 2021.

Kamworor ambaye ni bingwa mara mbili wa dunia katika mbio za nyika na mfalme mara mbili wa New York Marathon (2017 na 2019), amekuwa nje ya ulingo wa mashindano kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita kutokana na jeraha alilolipata baada ya kuhusika kwenye ajali ya pikipiki katika Kaunti ya Uasin Gishu.

Watimkaji wengine ambao wamejumuishwa kwenye orodha ya washiriki wa kipute cha RAK Half Marathon ni Reuben Kiprop Kipyego ambaye atakuwa akinogesha mbio za kilomita 21 kwa mara ya kwanza.

Kipyego alisajili muda wake bora wa binafsi wa saa 2:04:12 mnamo Oktoba 2020 aliposhiriki mbio za Valencia Marathon nchini Uhispania.

Mwanariadha huyo alishinda pia mbio za Abu Dhabi Marathon mnamo 2019 na ameapa kuwatoa kijasho Kamworor na mshikilizi wa rekodi ya dunia kwenye Nusu Marathon, Kibiwott Kandie.

Wakenya hao watatifuana na Waethiopia Shura Kitata na Jemal Yimer wanaopigiwa upatu wa kutia fora kwenye mbio hizo. Kitata anayejivunia muda bora wa binafsi wa dakika 59:47 kwenye mbio za kilomita 21, aliibuka mshindi wa London Marathon mnamo Oktoba 4, 2020.

Kwa upande wake, Yimer anajivunia muda bora wa binafsi wa dakika 58:33 na anashikilia nafasi ya pili duniani kwenye riadha za barabarani. Kwa sasa, ndiye mshikilizi wa rekodi ya kitaifa kwenye mbio za kilomita 21 nchini Ethiopia.

Mbio hizo za RAK Half Marathon zimewavutia pia wanariadha Yeman Crippa na Eyob Faniel. Crippa ambaye ni mzawa wa Ethiopia na raia wa Italia ndiye kwa sasa mshikilizi wa rekodi ya kitaifa kwenye mbio za mita 3,000, mita 5,000 na mita 10,000 nchini Italia.

Isitoshe, ndiye aliyetawazwa mshindi wa nishani ya shaba kwenye mbio za mita 10,000 kwenye mashindano ya bara Ulaya mnamo 2018 na akatia kibindoni medali ya fedha kwenye mbio za nyika barani Ulaya mnamo 2019.

Kwa upande wa wanawake, Obiri atatumia mbio hizo za RAK kujitosa rasmi kwenye kivumbi cha nusu marathon.

Mwanariadha huyo anajivunia nishani ya fedha kwenye mbio za kilomita 5,000 katika Olimpiki za 2016 jijini Rio, Brazil na ndiye mshindi wa zamani wa dunia katika mbio za mita 3,000 na mita 5,000. Aidha, ndiye bingwa wa Jumuiya ya Madola na bara la Afrika kwenye mbio za mita 5,000.

Mnamo 2020, Obiri alisajili muda wa dakika 30:53 kwenye mbio za kilomita 10 za barabarani jijini Barcelona, Uhispania na akaibuka mshindi licha ya kuanguka baada ya hatua ya kilomita tano.

Muda wake wa dakika 14:18.37 aliousajili kwenye mbio za mita 5,000 mnamo 2017 jijini Roma, Italia ndio wa sita kwa kasi zaidi duniani katika fani hiyo. Obiri ameapa kutumia mbio za RAK Half Marathon kuvunja rekodi ya dunia ya Nusu Marathon inayoshikiliwa na Mkenya Brigid Kosgei.

  • Tags

You can share this post!

NASAHA: Tusaidie katika kutambua na kukuza talanta za...

BBI: Mpira sasa waelekezwa kwa mabunge ya kaunti