• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 AM
Inter wabandua AC Milan kwenye Coppa Italia huku kigogo Zlatan Ibrahimovic akila kadi nyekundu

Inter wabandua AC Milan kwenye Coppa Italia huku kigogo Zlatan Ibrahimovic akila kadi nyekundu

Na MASHIRIKA

CHRISTIAN Eriksen alifungia Inter Milan bao la ushindi mwishoni mwa kipindi cha pili na kusaidia waajiri wake kusajili ushindi wa 2-1 dhidi ya AC Milan kwenye gozi la Coppa Italia lililoshuhudia Zlatan Ibrahimovic wa AC Milan na Romelu Lukaku wa Inter wakidhihirisha utovu wa nidhamu.

Wawili hao walizozana pakubwa uwanjani na refa akalazimika kumwonyesha Ibrahimovic kadi nyekundu iliyomfurusha uwanjani katika dakika ya 58.

Eriksen ambaye ni kiungo wa zamani wa Tottenham Hotspur alitokea benchi na kufunga frikiki iliyoshuhudia Inter wakitoka nyuma na kufuzu kwa nusu-fainali za Coppa Italia msimu huu.

Ibrahimovic aliwaweka AC Milan kifua mbele kunako dakika ya 31 kabla ya Lukaku kusawazisha mambo katika dakika ya 71 kupitia mkwaju wa penalti. Bao la Ibrahimovic ambaye ni raia wa Uswidi, lilikuwa lake la nane kutokana na mechi saba zilizopita dhidi ya Inter.

Ibrahimovic alionyeshwa kadi ya kwanza ya manjano kwa kumchezea Lukaku visivyo mwishoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya kuonyeshwa kadi ya pili ya manjano kwa kumkabili vibaya beki wa zamani wa Manchester City, Aleksandar Kolarov, dakika 13 baada ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa kipindi cha pili kupulizwa.

Penalti iliyofungwa na Lukaku ilichangiwa na tukio la Rafael Leao kumchezea visivyo Nicolo Barella ndani ya kijisanduku.

Bao la Eriksen aliyemtatiza pakubwa kipa Ciprian Tatarusanu wa AC Milan, lilikuwa lake la kwanza msimu huu baada ya kupangwa kwenye kikosi cha kwanza mara nne pekee muhula huu. Inter kwa sasa watakutana na mshindi wa robo-fainali nyingine itakayowakutanisha Juventus na SPAL mnamo Januari 27.

Kutowajibishwa sana kwa Eriksen kambini mwa Inter Milan wanaotiwa makali na kocha Antonio Conte kunatarajiwa kuwa kiini cha kuondoka kwa sogora huyo raia wa Denmark anayemezewa mate na Real Madrid ya Uhispania na Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa.

  • Tags

You can share this post!

BBI: Mpira sasa waelekezwa kwa mabunge ya kaunti

Manchester City waponda West Brom na kutua kileleni mwa...