• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
Manchester City waponda West Brom na kutua kileleni mwa jedwali la EPL

Manchester City waponda West Brom na kutua kileleni mwa jedwali la EPL

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City walipaa hadi kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa alama 41 baada ya kuwaponda West Bromwich Albion ya kocha Sam Allardyce 5-0 uwanjani The Hawthorns.

Hakuna timu nyingine katika Ligi Kuu tano za bara Ulaya ambayo imewahi kufungwa idadi kubwa ya mabao nyumbani kuliko West Brom waliomfuta kazi kocha Slaven Bilic mnamo Disemba 16, 2020.

Mabao ya Man-City dhidi ya West Brom yalipachikwa wavuni na Joao Cancelo, Riyad Mahrez, Raheem Sterling na Ilkay Gundogan aliyefunga mawili.

Ni pengo la alama moja kwa sasa ndilo linatenganisha Man-City na nambari mbili Manchester United. Leicester wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 38, tatu zaidi kuliko West Ham United wanaofunga mduara wa nne-bora. Mabingwa watetezi Liverpool walishuka hadi nafasi ya tano kwa pointi 34.

Kushindwa kwa West Brom kuliwasaza katika nafasi ya 19 jedwalini kwa alama 11, sita mbele ya Sheffield United wanaovuta mkia. Man-City ya kocha Pep Guardiola ilikosa huduma za wanasoka Kevin de Bruyne na Sergio Aguero katika mechi hiyo huku fowadi Gabriel Jesus akiletwa uwanjani mambo tayari yakiwa 5-0. Ushindi huo ulikuwa wa 11 mfululizo kwa Man-City kusajili katika kampeni za EPL msimu huu.

West Brom walishuka dimbani kwa minajili ya mchuano huo wakipigiwa upatu wa kutumia vyema uwanja wao wa nyumbani baada ya kuwalazimishia Man-City sare ya 1-1 wiki sita zilizopita uwanjani Etihad. Kipa Sam Johnstone wa West Brom alitamba sana katika mechi hiyo.

Katika mechi tano zilizopita ligini, West Brom wamefungwa jumla ya mabao 22, hii ikiwa idadi kubwa zaidi kwa kikosi cha EPL kupokea tangu Aston Villa ifanye hivyo mnamo Disemba 1935.

“Yasikitisha kwamba vijana walizembea uwanjani na kuruhusu Man-City watamalaki mchezo kuanzia mwanzo hadi mwisho na kutuzidia maarifa katika kila idara. Sikuwahi kabisa kufikiria kwamba kikosi changu kingefungwa idadi hiyo ya mabao katika mchuano mmoja,” akasema Allardyce aliyemrithi Bilic mnamo Disemba 2020.

Allardyce ambaye pia amewahi kuwa kocha wa timu ya taifa ya Uingereza, alikataa kuhojiwa na wanahabari hadi mwishoni mwa kipindi cha saa moja ya kuzungumza kwanza na wanasoka wake.

West Brom kwa sasa wamepoteza mechi tano mfululizo za EPL nyumbani kwa mara ya kwanza tangu Disemba 2004.

Man-City wanakwea kileleni mwa jedwali la EPL kwa mara ya kwanza msimu huu na ndiyo klabu ya tisa kufanya hivyo msimu huu. Mara ya mwisho kwa vikosi tisa kubadilishana uongozi wa jedwali la EPL kabla ya kutamatika kwa kampeni za msimu mmoja ni 1986-87.

Ni mara ya kwanza kwa Man-City kushinda mechi saba mfululizo za EPL tangu Agosti 2019. Allardyce anakuwa kocha wa kwanza baada ya Chris Ramsey aliyekuwa Queens Park Rangers (QPR) mnamo 2015 kupoteza mechi nne za kwanza za EPL nyumbani.

West Brom kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Fulham mnamo Januari 30 huku Man-City wakialika Sheffield United uwanjani Etihad siku hiyo.

MATOKEO YA EPL (Januari 26):

Crystal Palace 2-3 West Ham

Newcastle 1-2 Leeds United

Southampton 1-3 Arsenal

West Brom 0-5 Man-City

You can share this post!

Inter wabandua AC Milan kwenye Coppa Italia huku kigogo...

Hasla bandia, Joshua feki 2022?