KAMAU: Kapedo: Vijana wakabili desturi zinazowadunisha

Na WANDERI KAMAzU

UTOTONI mwetu, miongoni mwa hadithi ambazo mababu zetu walitutambia ni kuhusu jinsi walikuwa wakipanga njama za kuiba mifugo kutoka kwa jamii walizopakana nazo.

Hawangeutekeleza uvamizi huo vivi hivi tu. Ulikuwa mpango ambao ulipangwa kwa muda mrefu kwa kuwashirikisha wazee na vijana.

Vijana ambao walitwikwa jukumu hilo walipewa maagizo na mashauri na wazee hao kuhusu kanuni ambazo wangefuata kwenye harakati hizo.

Walipewa maelekezo kuhusu njia ambazo wangefuata, wakati mwafaka ambao wangevamia vijiji vya jamii husika na mbinu ambazo wangetumia kwenye uvamizi huo ili kuhakikisha walipata mifugo wengi zaidi.

Mashauri hayo pia yalijumuisha namna ambavyo wangepata mateka kutoka kwa jamii hizo, ikiwa uvamizi wao ungefaulu.

Bila shaka, hizo ndizo simulizi ambazo zilituchangamsha sana, hasa nyakati za jioni kabla ya chajio kuiva.

Ni matukio ya karne nyingi zilizopita. Kabla ya mauko yake, babu alitwambia kwamba huo ndio ulikuwa mkondo wa kimaisha enzihizo, ila hali imebadilika.

“Ushauri nitakaotoa kwenu wajukuu wangu ni kuwa kinyume na enzi zetu, silaha ya pekee kuyakabili maisha ya sasa ni elimu. Kamwe msiishi kama tulivyoishi. Tu vizazi viwili vilivyoishi katika nyakati tofauti sana. Zingatieni yaliyo muhimu na yanayoendana na maisha ya kisasa,” angeshauri babu.

Urejeleo huo unafuatia matukio ya kusikitisha yanayoendelea katika eneo la Kapedo, kwenye mpaka wa kaunti za Turkana na Baringo.

Kwa majuma kadhaa sasa, eneo hilo limegeuka kuwa ngome ya vita. Limegeuka kuwa uwanja wa fujo, vilio, majeraha na maafa. Ni mateso tu!

Katika dunia inayoendesha shughuli zake kwa mtandao na teknolojia ya kisasa, wezi wa mifugo wamelirejesha eneo hilo katika karne ya 18. Kinaya kilichoje!

Inasikitisha kuwa jamii zinazoishi eneo hilo bado zinachukulia wizi wa mifugo kama vitendo vya “ushujaa.”

Kufikia sasa, zaidi ya watu kumi wameuawa, miongoni mwao wakiwemo polisi na wanataaluma wengine waliotumwa kutuliza hali.

Kama hayo hayatoshi, ripoti za kijasusi zinasema baadhi ya viongozi wa kisiasa wanahusika kwenye ufadhili wa vitendo hivyo. Hili ni sikitiko kuu.

Huu ni usaliti. Ikiwa huo ndio ukweli, wanasiasa hao wanavisaliti vizazi vya sasa ambavyo vingezisaidia jamii zao kujikomboa dhidi ya tamaduni hizo zilizopitwa na wakati.

Kufadhili vitendo hivyo ni sawa na kuwapumbaza vijana wasitambue uwezo walio nao kwa kushiriki kwenye shughuli zitakazojenga maisha yao. Ilivyo sasa, miongoni mwa sekta zilizoathiriwa sana ni elimu.

Shule zote zimefungwa huku walimu wachache waliopo wakitishia kuondoka. Serikali nayo imesimama kidete ikisema kuwa, itawalazimu wenyeji kuwafunza watoto wao hali ya kawaida itakaporejea.

Katika patashika hii yote, vijana ndio wanatiwa utumwani. Utumwa wa kutofunguka macho na utumwa wa tamaduni za kikale. Huo si ‘ushujaa’ kamwe!

Ni wakati vijana hao wazinduke na kufahamu kuwa ‘ushujaa’ halisi katika enzi ya sasa ni kupitia elimu pekee.

Ni kupitia ufahamu huo watakapobaini wanasiasa wanowafadhili ndio maadui wao wakuu!

akamau@ke.nationmedia.com

Habari zinazohusiana na hii