BBI: Kizaazaa Raila akizuru Githurai
Na SAMMY WAWERU
KIZAAZAA kimeshuhudiwa Jumatano katika mtaa wa Githurai kufuatia ziara ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga kupigia debe Ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI).
Makundi mawili hasimu ya vijana yalikabiliana vikali kwa kurushiana mawe na matawi ya miti.
Bw Raila alipotua, alihutubia wafanyabiashara wa soko la Migingo kwa utulivu, akiahidi kushinikiza serikali kuwaimarishia mazingira ya kazi.
“Nimepokea malalamishi ya wafanyabiashara na ninawahakikishia yatafikia ndugu yangu Rais Uhuru Kenyatta,” Bw Raila akaambia wafanyabiashara na wachuuzi wa Migingo.
Hata hivyo, vurugu zilizuka wakati akihutubia wachuuzi wa soko la Jubilee, lililoko mita chache kutoka lile la Migingo.
Ghasia hizo zilichochewa na kundi la vijana wanaodaiwa kuhusishwa na Naibu wa Rais, Dkt William Ruto, waliotaja na kukariri majina ya Ruto na kubeba toroli wakati kiongozi wa ODM akizungumza.
Juhudi za Bw Raila kujaribu kuwahutubia hata hivyo ziligonga mwamba, kilele kikawa makundi (moja linalohusishwa na Ruto na lingine Raila) hayo kukabiliana.
Maafisa wa polisi walilazimika kutumia gesi ya vitoa machozi kutuliza mapigano.

Kulingana na baadhi ya wafanyabiashara wa soko la Jubilee waliozungumza na Taifa Leo, walieleza kughadhabishwa kwao na madai ya utapeli wa soko jipya linalotengenezwa, unaosakatwa na wahuni.
“Tumearifiwa Raila Odinga alialikwa na watu wanaotaka kutwaa soko letu, tunaotengenezewa tukose nafasi. Hilo halitawezekana,” akasema mfanyabiashara mmoja.
Biashara nyingi hazikufunguliwa Jumatano asubuhi na zilizoendeleza huduma zikilazimika kufunga, kufuatia hofu ya vurugu kuzuka.
Soko jipya linalotengenezwa linakadiriwa kusitiri wafanyabiashara 1,500 pekee.
Akizungumza katika soko la Migingo, Bw Raila aliahidi kwamba wachuuzi ambao hawatapata nafasi watatafutiwa sehemu mbadala kujiendeleza kimaisha.
Kiongozi huyo wa ODM alikuwa ameandamana na Seneta wa Siaya Bw James Orengo, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, mbunge maalum Bw Maina Kamanda na Mbunge wa Likoni Mishi Mboko miongoni mwa viongozi wengine.