COVID-19: Mmoja afariki, serikali yathibitisha visa vipya 130

Na CHARLES WASONGA

MTU mmoja pekee ndiye amethibitishwa kufariki kutokana na corona Jumatano huku watu 130 wapya wakipatikana na ugonjwa huo nchini Kenya.

Kifo hicho kimefikisha idadi jumla wa waliofariki kufikia siku hiyo kuwa 1,751 huku idadi jumla ya maambukizi ikifika 100,323.

Visa hivyo 130 vipya viligunduliwa kutokana na sampuli 4,918 zilizopimwa na hivyo kufikisha idadi jumla ya vipimo kuwa 1,167,409 tangu kisa cha kwanza cha corona kilipogunduliwa nchini mnamo Machi 13, 2020.

Visa hivyo vipya vya maambukizi vimesambazwa jinsi ifuatavyo; Nairobi 66, Taita Taveta 18, Mombasa 9, Nakuru 6, Narok 6, Siaya 4, Uasin Gishu 4, Kiambu 4, Kisii 4, Kilifi 2, Kisumu 1, Bungoma 1, Busia 1, Kajiado 1, Kakamega 1, Nyamira 1 na Nyandarua 1.

Kwenye taarifa aliyoituma kwa vyombo vya habari Waziri wa Afya Mutahi Kagwe ameongeza kuwa idadi jumla ya wagonjwa waliothibitishwa kupona sasa imetimu 83,691 baada ya wagonjwa 66 zaidi kupona na kuruhusiwa kurejelea maisha yao ya kawaida.

“Miongoni mwa waliopona, 42 walikuwa chini ya mpango wa uuguzi nyumbani ilhali 24 walikuwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali za humu nchini,” akaeleza katika taarifa hiyo.

Bw Kagwe pia ameongeza kuwa jumla ya wagonjwa 489 wakati huu wamelazwa katika vituo mbalimbali vya afya huku 1,353 wakiuguzwa nyumbani.

Wagonjwa 20 wa corona nao wamelazwa katika vyumba vya kuwahudumia wagonjwa mahututi (ICU) huku 14 wakisaidiwa kupumua kwa mitambo ya “ventilators”. Wagonjwa wengine 13 wanaongezwa oksijeni.

Habari zinazohusiana na hii

Dkt Mogusu atawagusa?