• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:03 PM
Kalonzo ajizolea sifa ya tikitimaji

Kalonzo ajizolea sifa ya tikitimaji

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa Wiper, Kalonzo Musyoka ndiye anayefahamika zaidi nchini kwa kudandia umaarufu wa wanasiasa wenzake kupata madaraka.

Wadadisi wa siasa wanasema Bw Musyoka ni mnyonge katika kufanya maamuzi yanayostahili kumwezesha kushinda urais.

Hata hivyo, wanaomfahamu wanasema kwamba Bw Musyoka huwa anachukua muda kabla ya kufanya uamuzi, na anapoufanya huwa anaangukia kambi anayoonelea ni yenye nguvu za kushinda.

“Bw Musyoka hajitokezi kwa nguvu kutetea wananchi, jambo ambalo linazima umaarufu wake katika maeneo mengine ya nchi mbali na ngome yake ya Ukambani,” asema mwanasiasa mmoja wa Machakos mwandani wa Bw Musyoka.

Bw Musyoka alipojiunga na siasa mnamo 1983, alitegemea ushawishi wa aliyekuwa msemaji wa jamii ya Wakamba wakati huo, Mzee Mulu Mutisya aliyemtambulisha kwa Rais Daniel Moi.

Ingawa Mzee Moi alimteua kusimamia wizara muhimu katika serikali yake, Bw Musyoka analaumiwa kwa kutosaidia eneo la Ukambani kustawi, madai ambayo amekuwa akikanusha.

Bw Musyoka alihama Kanu mnamo 2002 uongozi wa Moi ukielekea ukingoni na kujiunga na Raila Odinga na George Saitoti miongoni mwa wengine kuunda Rainbow Alliance, vuguvugu ambalo liliungana na muungano wa National Alliance Kenya (NAK) kubuni muungano wa National Rainbow Alliance (NARC) uliotamatisha uongozi wa chama cha Kanu.

Wachanganuzi wa siasa wanasema kwamba tangu 2002, Bw Musyoka amekuwa akitegemea umaarufu wa vigogo wa kisiasa akiwemo Bw Odinga, Mzee Kibaki na hata Rais Uhuru Kenyatta kubaki katika siasa za kitaifa.

“Hii ndiyo ilimfanya apachikwe jina la tikitimaji kwa kutokuwa na msimamo thabiti. Nafikiri huwa anadandia upande unaoweza kumfaa zaidi na hiyo ni kawaida ya siasa,” asema mchanganuzi wa siasa, Geff Kamwanah.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2007, Bw Musyoka alitarajia kuwa Bw Odinga angemuidhinisha kuwa mgombea urais wa chama cha Orange Democratic Kenya (ODM-K) na alipokataa alihepa na cheti cha chama hicho.

Alitumia chama hicho kugombea urais mwaka huo na akadandia utata uliozuka kufuatia uchaguzi huo kwa kuungana na Mzee Kibaki aliyemteua makamu rais.

Alitarajia kuwa Mzee Kibaki angemuunga mkono kuwa mrithi wake kwenye uchaguzi mkuu wa 2013 lakini akaachwa kwenye mataa.

Bw Musyoka aliyebadilisha jina la ODM-K kuwa Wiper, alilazimika kuungana na Bw Odinga kuokoa nyota yake ya kisiasa wakaunda muungano wa Coalition for Restoration of Democracy (Cord) ulioshirikisha kiongozi wa chama cha Ford Kenya, Moses Wetangula.

Kwenye uchaguzi wa 2017, alikuwa mmoja wa vinara watano wa muungano wa NASA ambao alitarajia kuwa Bw Odinga angemuunga mkono lakini hakutoboa.

Mnamo 2018 alijitangaza kuwa ‘mtu wa mkono’ wa Rais Uhuru Kenyatta, hatua ilitajwa kuwa mbinu ya kujipendekeza kwa rais.

“Kuanzia leo, nitakuwa mtu wa mkono wa rais na sitaki kuulizwa maswali,” alitangaza mbele ya viongozi waliohudhuria mazishi ya babake.

Bw Musyoka aliteuliwa balozi wa amani nchini Sudan Kusini muda mfupi baada ya kujiita ‘mtu wa mkono wa rais’, wadhifa anaofurahia wakati huu.

You can share this post!

Vijana wavuruga mkutano wa kupigia debe BBI alioongoza Raila

Muthama, mkewe wa zamani waanza kuraruana kisiasa