Magufuli adai chanjo ya kigeni imeingiza corona mpya Tanzania

Na MWANDISHI WETU

DAR ES SALAAM, Tanzania

RAIS John Pombe Magufuli, sasa amelaumu watu waliopokea chanjo dhidi ya virusi vya corona nje ya nchi akidai wameingiza aina mpya ya Covid-19 nchini humo.

Akizungumza Jumatano, Rais Magufuli alitilia shaka chanjo zilizotengenezwa kufikia sasa na akawaonya raia wake wasikimbilie kupewa chanjo hizo.

“Mtatishwa sana ndugu zangu Watanzania lakini simameni imara, najua wapo baadhi ya Watanzania hata wameondoka nchini kukimbilia maeneo mengine na kuenda kuchanjwa na walikochanjwa huko wamekuja huku wametuletea corona ambayo ni ya ajabuajabu. Simameni imara,” akasema.

Matamshi yake yalijiri wakati ambapo kuna wasiwasi miongoni mwa baadhi ya raia kuhusu kuchipuka kwa wimbi jipya la maambukizi ya virusi vya corona Tanzania.

Serikali ya Tanzania imekuwa ikisisitiza kuwa taifa hilo halina visa vyovyote vya corona kwani walifanikiwa kushinda janga hilo kupitia kwa maombi na kinga za mitishamba.

“Chanjo hazifai. Iwapo Wazungu wangekuwa na uwezo wa kuleta chanjo, hata chanjo ya Ukimwi ingekuwa imeshaletwa, chanjo ya kifua kikuu ingekuwepo na maradhi hayo kuondoka, hata chanjo ya malaria ingekuwa ishapatikana na hata chanjo ya kansa ingekuwa imeshapatikana. Lazima Watanzania tuwe waangalifu dhidi ya mambo ya kuletewa kutoka ughaibuni,” akasema Magufuli.

Hivi majuzi, Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) lilitoa tahadhari kwa washiriki wa kanisa hilo kuwa waangalifu dhidi ya kuambukizwa virusi hivyo.

Mkuu wa TEC, Askofu Gervas Nyaisonga, alisema juhudi ambazo zimewekwa na serikali kukabili kuenea kwa virusi hivyo tangu Machi mwaka uliopita zimeonyesha dalili za kufaulu, ila taifa hilo sasa linakumbwa na wimbi jipya la maambukizi.

“Mwaka 2020 maambukizi yalishuka sana na tuliamini tumefanikiwa kulikabili janga hilo. Nchi yetu si tofauti. Lazima tuchukue tahadhari za kutosha na kumwomba Mungu atulinde ili kutoathiriwa na janga hili,” akasema kwenye taarifa.

Wiki iliyopita, mwanafunzi kutoka Shule ya Kimataifa ya Moshi (ISM) alipatikana na virusi, hali iliyoufanya usimamizi wa shule hiyo kuifunga mara moja.

Hata hivyo, Mshirikishi Mkuu wa eneo la Kilimanjaro, Anna Mghwira, alipinga taarifa hizo zilizokuwa zimechapishwa katika mtandao wa shule husika.

Wasimamizi wa taasisi hiyo walilazimika kuomba msamaha kwa ripoti hizo.

Vile vile, serikali ya Uingereza ilipiga marufuku watu wanaotoka Tanzania kuingia nchini humo. Raia wa Uingereza wanaotokea Tanzania watalazimika kukaa karantini siku kumi.

Serikali ya taifa hilo sasa imewaomba raia wake kuwa wenye utulivu na kungoja mwelekeo rasmi utangazwe kuhusu janga hilo.

Habari zinazohusiana na hii