TAHARIRI: Fujo hizi za kisiasa hazifai kuvumiliwa

KITENGO CHA UHARIRI

VURUGU zilizoshuhudiwa Jumatano wakati wa mkutano wa hadhara ulioongozwa na Kiongozi wa ODM Raila Odinga katika eneo la Githurai, Nairobi, hazikushangaza watumizi wa mitandao ya kijamii walio makini.

Hii ni kutokana na kuwa, ndimi za uchochezi zilielekezwa katika mitandao ya kijamii mapema na dalili zilionyesha wazi uwezekano wa mashambulio katika mkutano huo.

Tangu mapema asubuhi, wafuasi wa pande tofauti za kisiasa walikuwa wanajibizana kwa maneno makali katika mitandao ya kijamii kuhusu ziara ya Bw Odinga.

Bw Odinga alikuwa katika eneo hilo kuvumisha Mswada wa Maridhiano (BBI) ambao umefikia hatua ya kujadiliwa na mabunge ya kaunti kabla ya kura ya maamuzi kufanywa baadaye.

Inatarajiwa mikutano sawa na hiyo itaendelea kuandaliwa katika maeneo mengine ya nchi kuendelea mbele.

Matamshi ya uchochezi na migawanyiko ambayo yamekuwa yakienezwa katika mitandao ya kijamii kwa muda sasa, ni ya kutisha.

Hayo yanaongeza tishio ambalo tayari lipo kutoka kwa ndimi za baadhi ya wanasiasa ambao kila wanaposimama kuzungumza, hakuna chochote cha maana wanachosema isipokuwa kugawanya taifa kwa mirengo tofauti.

Taifa lisipozinduka mapema na kuzima matukio haya sasa hivi, tutajutia kimya chetu katika miezi michache ijayo tunapoelekea katika Uchaguzi Mkuu.

Kila mara wito hutolewa kwa vijana ambao ndio wengi wanaotumiwa vibaya na wanasiasa, wakome kukubali pesa nane wanazolipwa kwenda kuzua vurugu za kisiasa.

Inavyoonekana, juhudi hizo za kuhamasisha vijana kuhusu umuhimu wa kufuata viongozi walio na sera bora za uongozi zimegonga mwamba.

Kando na kutumiwa vibaya kurusha mawe na kushambulia watu katika mikutano ya siasa, ni wao hao wanaotumiwa kueneza habari na jumbe za uchochezi kupitia kwa mitandao yao ya kijamii.

Kwa upande mwingine, sheria zinazofaa kuwaadhibu wanasiasa wachochezi na vile vile raia wa kawaida wanaoeneza uchochezi, zinaonekana kuwa dhaifu.

Matukio kama haya ambapo uchochezi unaenezwa kwa kasi zaidi kupitia mitandao ya kijamii ndiyo hutoa mwanya kwa viongozi wa kiimla katika baadhi ya mataifa ya nje kuzima mitandao wakati kampeni za kisiasa zinapokaribia kushika moto.

Dalili za vurugu zimekuwepo humu nchini kwa muda sasa, lakini inavyoonekana, wadau husika wameamua kulifumbia macho suala hilo.

Habari zinazohusiana na hii