• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:10 PM
AKILIMALI: Jinsi teknolojia inavyopunguza gharama ya kukuza kabichi na pilipili maeneo kame

AKILIMALI: Jinsi teknolojia inavyopunguza gharama ya kukuza kabichi na pilipili maeneo kame

Na GRACE KARANJA

KILIMO cha aina tofauti za mboga katika baadhi ya mataifa ni rahisi kwani hakihitaji maelfu ya ekari za mashamba ili kufanikisha.

Aina nyingi za mboga huliwa na wengi wa Wakenya kama chakula chao cha kila siku huku wataalamu wa lishe wakiwahimiza watu kula mboga kwa wingi ili kujiepusha na magonjwa ambayo yanaweza kuzuiliwa na ulaji wa mboga. Kabichi na pilipili mboga ni mfano tu wa mboga ambazo huliwa ama kwa njia ya kupikwa au zikiwa mbichi kama kachumbari.

Aina hii ya mboga huwa katika makundi mawili: zile zilizo na vichwa vidogo na vya wastani ambazo hufaa katika masoko ya wazi. Kundi la pili ni la vichwa vikubwa ambazo soko lake huwa ni hospitali, shule na katika hoteli. Zao hili linahitaji kunyunyiziwa maji ili kuwa na matawi yenye afya ambayo hutengeneza vichwa vyake. Kabichi huhitaji mililita 500 za maji hivyo kama eneo unalolima halina maji ya kutosha, mkulima atahitajika kutimia mbinu mbadala kama vile mfumo wa unyunyiziaji maji kwa njia ya matone, njia za kunyunyizia kwa mitaro na nyinginezo. Njia hizi hufanya vichwa vya kabichi kukua kwa ukubwa na kwa saizi moja pamoja na kuzuia vichwa hivi kupasuka.

Zao la kabichi ukanda wa Afrika Mashariki hukuzwa katika mataifa ya Uganda, Tanzania na Kenya. Wakulima wale wa ngazi za chini na wakulima walio na mashamba makubwa.

Hapa nchini Kenya, kwa miaka mingi, wengi huamini kuwa zao hili hukuzwa katika maeneo yaliyo na baridi na unyevunyevu wa udongo. Lakini sasa wataalamu wanawashauri wakulima walio na vitovu vya maji hasa katika maeneo kavu kujaribu kukuza aina hii ya mboga.

Njia mojawapo ya kukuza mazao katika maeneo kavu na yaliyo na jua kali kama vile Mashariki na Kaskazini mashariki ni kuchimba visima virefu vya maji na kutumia njia ya matone ya kunyunyizia mimea.

Aidha wataalamu na kampuni mbalimbali hapa nchini na pia ulimwenguni zimeibuka na mbinu za kisasa ya kukuza mimea kwa kutumia karatasi maalumu almaarufu mulching film/paper. Karatasi hii ina manufaa yake katika uhifadhi wa udongo na ustawi wa mimea.

Kabla ya kupanda aina yoyote ya mmea, lazima mkulima achukue jukumu la upimaji wa udongo; hii ikiwa ni njia ya kufahamu madini yanayopungua katika udongo huo.

“Wakulima wanaweza kukuza mazao bila kujali hali ya hewa kwani mboga nyingi hazichagui aina ya udongo na hewa ikizingatiwa kuwa udongo ulio na tindikali kati ya 5.5-6.5 hufaa kwa baadhi ya mimea,” anaeleza mtalamu, mwanzilishi na mshauri kutoka kampuni ya Maishamba Agro Solutions Ltd, Vonnies Onkoba.

Kwanza kabisa, karatasi hii ya plastiki husaidia kuhifadhi unyevu katika udongo kwa mfano katika maeneo ambayo hupokea viwango vya chini vya mvua. Hivyo, husaidia mkulima kupunguza unyunyiziaji wa maji mara kwa mara na kumpa muda wa kufanya kazi nyinginzo. Karatasi hii inaweza kutumika wakati mkulima ananyunyizia maji mimea kwa njia ya matone yaani drip irrigation. Karatasi hii pia hupunguza gharama ya upalizi kwani hudidimiza uwezekano wa magugu kuota ambayohuleta ushindani mkubwa wa lishe kati ya mimea ya mazao na magugu.

Pia hupunguza gharama ya unyunyiziaji madawa ya kuua wadudu ambayo huharibu matunda au majani yam mea maalum shambani. Karatasi hii huwanyima wadudu hewa kwani hawawezi kukaa chini yake, hivyo mmea unapata nafasi ya kukua bila kudidimia.

“Ili karatasi hii kutumika vitalu hutengenezwa na udongo kuchanganywa na mbolea aina ya samadi iliyooza vizuri kwani husaindia ukuwaji wa haraka wa mmea na wenye afya. Kisha mifereji ya maji ya matone huwekwa chini katika vipimo nafasi ya mimea kutoka mstari mmoja hadi mwingine. Kisha inawekwa juu ya kitalu na kutombolewa kwa mkono nafasi ya mviringo ambayo hupandwa mmea.

Licha ya kupunguza gharama ya uzalishaji karatasi hii inaweza kukaa kati ya miaka miwili na mitano kulingana na upana wake wa maikromita. Bei ya kununua karatasi hii hulingana na mfuko wa mkulima kwa mfano kuna ile ambayo huuzwa mita 1,000 mraba kwa Sh44,000.

You can share this post!

BONGO LA BIASHARA: Jinsi video, picha zilivyomsukuma...

AKILIMALI: Mboga ainati za kiasili ndizo tegemeo la riziki