• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 5:29 PM
Leicester City na Everton nguvu sawa ligini

Leicester City na Everton nguvu sawa ligini

Na MASHIRIKA

LEICESTER City walidhihirisha kwamba wao ni miongoni mwa wagombezi halisi wa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kwa kutoka nyuma na kuwalazimishia Everton sare ya 1-1 mnamo Jumatano usiku uwanjani Goodison Park.

Licha ya kuanza mechi hiyo kwa matao ya juu na kumiliki asilimia kubwa ya mpira katika kipindi cha kwanza, vijana wa kocha Brendan Rodgers walijipata nyuma kupitia bao la James Rodriguez aliyefungia Everton katika dakika ya 30 kwa kuvurumisha fataki kutoka hatua ya 20.

Wenyeji Everton walikamilisha kipindi cha kwanza wakiwa kileleni kabla ya Leicester waliomweka kipa Jordan Pickford katika ulazima wa kufanya kazi ya ziada katika kipindi cha pili kusawazisha mambo kupitia Youri Tielemans.

Bao hilo la Tielemans lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na viungo Yerry Mina na James Maddison.

Goli hilo liliwapa Leicester ari ya kuendea ushindi ila juhudi zao zikakosa kuzaa matunda huku Everton nao wakipoteza fursa nzuri za kufunga mabao mawili mwishoni mwa kipindi cha pili kuitia kwa Richarlison Andrade na Dominic Calvert-Lewin.

Sare iliyosajiliwa na Leicester dhidi ya Everton iliwasaza katika nafasi ya tatu kwa alama 39, mbili pekee nyuma ya viongozi Manchester City. Ni pengo la alama moja pekee ndilo linawatenganisha Leicester na Man-United ambao pia ni wagombezi halisi wa taji la EPL msimu huu licha ya kupokezwa kichapo cha 2-1 kutoka kwa Sheffield United mnamo Jumatano usiku ugani Old Trafford.

Kwa upande wao, Everton wanaonolewa na kocha Carlo Ancelotti, wanakamata nafasi ya saba kwa alama 33 sawa na Tottenham Hotspur watakaokuwa wenyeji wa Liverpool kwa gozi kali la EPL mnamo Januari 28.

Ni pengo la pointi mbili ndilo linawatenganisha Everton na West Ham United ambao chini ya kocha David Moyes, wanafunga orodha ya nne-bora kwa alama 35.

Everton kwa sasa wanajiandaa kualika Newcastle United uwanjani Goodison Park mnamo Januari 30 huku Leicester wakiwa wenyeji wa Leeds United ugani King Power siku moja baadaye.

You can share this post!

BBI yasababisha mpasuko miongoni mwa madiwani wa Mlima Kenya

Zaidi ya hospitali 17 za umma kuzinduliwa Nairobi