• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
Visa vya maambukizi ya corona duniani vyapindukia 100 milioni

Visa vya maambukizi ya corona duniani vyapindukia 100 milioni

CHARLES WASONGA na MASHIRIKA

VISA vya maambukizi ya virusi vya corona duniani Jumatano vilivuka watu milioni 100 huku mataifa kote ulimwenguni yakijipanga kukabiliana na aina mpya ya virusi hivyo na changamoto ya uhaba wa chanjo.

Idadi hiyo ya visa vya maambukizi ni sawa na asilimia 1.3 ya idadi jumla ya watu ulimwenguni ambao wameambukizwa na virusi hivyo vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.

Jumla ya watu 2.1 milioni, (inayowakilisha kiwango cha vifo cha asilimia 2.15) wameuawa na ugonjwa huo ambao uligunduliwa kwa mara ya kwanza katika mji wa Wuhan, China mnamo Desemba 15, 2020.

Tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 202 visa 668,250, kwa wastani, huripotiwa duniani kila siku, kulingana na takwimu zilizotolewa na shirika la habari la Reuters.

Mataifa ambayo yameathirika zaidi na janga hili la Covid-19 ni; Amerika, India, Brazil, Urusi na Uingereza, ambayo kwa pamoja yamechangia zaidi ya nusu ya visa vya ugonjwa huo kote duniani. Idadi jumla ya watu katika mataifa hayo inawakilisha asilimia 28 ya idadi ya watu ulimwenguni, kulingana na uchanganuzi wa shirika hilo la habari.

Karibu nchini 56 zimeanza kutoa chanjo dhidi ya corona kwa raia wao ambapo zimetoa angalau dozi 64 milioni kufikia Jumatano. Israeli ndio inaongoza katika idadi ya raia ambao wamepewa chanjo ambapo asilimia 29 wamepewa angalau dozi moja.

Amerika ambayo imeandikisha zaidi ya visa 25 milioni vya maambulizi imechangia asilimia 25 ya idadi jumla ya maambukizi ya Covid-19 duniani. Hii ni licha ya kwamba idadi ya watu nchini Amerika inawakilisha asimilia 4 pekee ya idadi jumla ya watu ulimwenguni.

Amerika pia inaongoza katika idadi ya wagonjwa ambao huripotiwa kufariki kila siku, ambapo inakadiriwa kuwa kati ya wagonjwa watano wanaofariki duniani kila siku, mmoja hutoka Amerika.

Kufikia Juamtano, Amerika ilikuwa imeandikisha karibu vifo 425,000 kutokana na corona, idadi ambayo ni mara mbili ya idadi ya vifo nchini Brazil ambayo imenakili idadi ya pili ya juu ya vifo.

Bara Uropa ambayo ndilo limeathirika zaidi duniani ambapo linaripoti visa milioni moja vipya kila baada ya siku nne. Bara hilo limethibitisha karibu visa 30 milioni vya maambukizi ya corona tangu janga hilo lilipolipuka duniani.

Mnamo Jumanne, Uingereza ilifikisha vifo 100,000 vya wagonjwa kutokana na ugonjwa huo.

Licha ya kutia saini mikataba ya usambazaji wa chanjo hapo awali, mengi ya mataifa ya bara Uropa yanakabiliwa na shida ya kucheleweshwa kwa uwasilishwa wa chanjo hizo kutoka kwa kampuni za dawa za Pfizer na AstraZeneca.

Katika taifa la India ambayo huandikisha katibu visa 13,700 vya maambukizi kila siku, limekuwa likiandikisha kupungua kwa idadi ya maambukizi mapya.

Waziri Mkuu wa nchini hiyo Narendra Modi Ijumaa alisema ndani ya muda wa wiki mmoja jumla ya watu milioni moja walikuwa wamepewa chanjo.

China ambayo juzi iliadhiminisha mwaka mmoja tangu ilipotangaza amri ya kutotoka nje (lockdown) Wuhan, imekuwa ikiandikisha visa vipya vya maambukizi ya corona.

Pengo

Japo mataifa tajiri yanajizatiti kuendesha kampeni ya utoaji chanjo, yale ya Afrika yanajizatiti kupata chanjo hiyo huku aina mpya ya virusi vya corona ikigunduliwa Afrika Kusini na Uingereza.

Kulingana na takwimu hizo za Reuters, mataifa ya Afrika yameandikisha jumla ya visa 3.5 milioni vya maambukizi na zaidi ya vifo 85,000.

Aina mpya ya virusi hivyo iliyogunduliwa Afrika Kusini, ambayo inaitwa 501Y.V2, inasambaa kwa hadi asilimia 50 zaidi ya aina ya kwanza iliyogunduliwa China. Aina hii mpya ya virusi vya corona tayari imesambaa katika karibu mataifa 20.

Kuanzia Jumamosi Rais wa Amerika Joe Biden alisema taifa lake litaanza kutekeleza amri ya kuzuia watu kutoka Afrika Kusini kuingia Amerika, ili kuzuia kuenea kwa aina hiyo mpya ya virusi.

You can share this post!

Kibarua cha kwanza cha kocha Tuchel kambini mwa Chelsea...

NOC-K yasambaza mavazi yaliyotoweka wakati wa Olimpiki za...