• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Presha kwa Raila akae kando 2022 aachie wengine

Presha kwa Raila akae kando 2022 aachie wengine

SHABAN MAKOKHA na MWANGI MUIRURI

SHINIKIZO zimezidi kutolewa na viongozi wa chama cha ODM zikimtaka kiongozi wa chama hicho, Bw Raila Odinga aweke kando maazimio yake ya kuwania urais ifikapo 2022.

Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya, anamtaka Rais Uhuru Kenyatta amshawishi Bw Odinga asiwanie urais katika uchaguzi unaotarajiwa mwaka ujao. Bw Oparanya alikariri kwamba atagombea urais naye Bw Odinga anafaa kumuunga mkono.

Wito huu wa Bw Oparanya umetokea wiki chache baada ya Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, pia kumtaka Bw Odinga aunge mkono Mpwani kwa urais katika uchaguzi ujao.

Bw Joho ambaye pia anamezea mate urais, alikuwa amesema kuwa eneo la Pwani limemuunga mkono Bw Odinga kwa muda mrefu, na anaamini anafaa ‘kurudisha mkono’.

Akizungumza katika ukumbi wa Mumias Cultural Center alipokutana na wahudumu wa afya wa kujitolea (CHVs) na vijana wanaoshiriki mpango wa Kazi Mtaani, Bw Oparanya alidai kwamba yeye ndiye anayeweza kumshinda Naibu Rais William Ruto.

Alisema kwamba alikutana na Rais Kenyatta Jumatano wiki jana na akamtuma kumshawishi Bw Odinga amuunge mkono.

“Nitawasilisha stakabadhi zangu kuomba tiketi ya chama cha ODM kugombea urais. Iwapo Bw Odinga ataniunga mkono, nina hakika nitamshinda Dkt Ruto kwa kura nyingi,” alisema.

“Nilimuomba Rais amshawishi Bw Odinga asigombee urais na kuniunga mkono. Sifanyi mzaha katika uamuzi huu ambao utapeleka Kenya katika kiwango cha juu katika uongozi barani Afrika na ninashauriana kwa mapana kuhusu hilo,” alisema.

Alipoulizwa iwapo atampinga Bw Odinga iwapo ataamua kugombea urais kwa mara nyingine, Bw Oparanya alisema “wakati utaamua.”

“Raila amekuwa baba yangu kisiasa na amenilea kisiasa tangu 2002. Ni kupitia mchango wa Raila ambapo nimeweza kufika nilipo. Lakini sasa wakati umefika wa mimi kupanda cheo na ninamuomba aniunge mkono,” aliongeza.

Wito sawa na huu wa kumtaka Bw Odinga aachie wengine nafasi 2022, umekuwa ukitolewa na waliokuwa vinara wenzake katika Muungano wa National Super Alliance (NASA). Hawa ni, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, mwenzake wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula (Ford Kenya).

Maelewano

Katika mahojiano kwenye redio Alhamisi, Bw Mudavadi alimkumbusha Bw Odinga kwamba walikuwa na maelewano katika NASA kuhusu uwaniaji urais.

“Hata unapoungana na Rais Kenyatta kutawala serikali ya Jubilee, bado wewe ni mwanachama wa NASA unayesimamiwa na makubaliano yetu ya kabla uchaguzi (wa 2017). Tulielewana tumuunge (Raila) kwa urais mwaka 2017 hadi 2022 pekee kisha baadaye aweke kando maazimio yake na kuunga mkono mmoja wetu katika NASA,” akasema Bw Mudavadi.

Bw Oparanya ambaye ni mwenyekiti wa baraza la magavana (CoG) anayeondoka, alisema alianza kushirikiana na Bw Odinga mwaka wa 2002 alipochaguliwa mbunge wa Butere kwa tiketi ya chama cha Narc.

Alimkumbusha Bw Odinga kwamba alibaki kiongozi wa pekee mwaminifu kwake katika jamii ya Waluhya ambaye amekuwa akiunga azma yake ya urais.

Alieleza, “Nimemsaidia kuungwa mkono nilipohudumu kama mbunge kwa mihula miwili na nimekuwa nikimuunga nikihudumu kama gavana wa Kakamega. Wakati umefika Bw Raila Odinga arudishe mkono kwa juhudi zangu kwa kuniunga mkono nimrithi Rais Kenyatta”.

Alisema kwamba jamii ya Waluhya ilimuunga Bw Odinga alipogombea urais 2007, 2013, na 2017 na akamtaka kiongozi huyo wa ODM kuwaongoza wafuasi wake kuirudishia mkono kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Chama cha ODM kimetangaza kuwa kimeanza kusaka mgombea wake wa urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

You can share this post!

Minisketi zasababisha mvutano Malindi

Murathe sasa akiri kauli ya Kang’ata ni kweli kuhusu BBI...