OMAUYA: Wachuuzi wa ahadi hewa wameanza kuingia mjini

Na MAUYA OMAUYA

WAJINGA ndio waliwao!

Hakuna anayeweza kutumia mgongo wako kwa starehe za mwendeshaji farasi ila kwa wewe mwenyewe kujipinda na kumwandalia mgongo! Iwapo wananchi wa taifa la Kenya watafahamu hili, watajiepusha na dhiki ya kusaga meno kwa kujikaanga kwenye hadaa hadaa za wanasiasa.

Ninasema hili kwa sababu, kila ishara inaonyesha kwamba soko la siasa nchini Kenya limefunguliwa rasmi. Wachuuzi ni wale wale, wanunuzi hawajabadilika na bidhaa ni zile zile. Wachuuzi wa siasa za Kenya wanatuuzia tiketi ya kusafiri hadi nchi iitwayo Utopia. Kumbuka, Utopia sio Ethiopia!

Utopia ni nchi ambayo kuwepo kwake hufikirika kwa mawazo tu, sio tofauti na ile aliyosimulia Shaaban Robert kwenye kitabu cha Kusadikika. Lakini simulizi za Utopia zimekuwepo kwa miaka na mikaka. Mwanafalsafa Plato wa Ugiriki alisimulia uwepo wa nchi iitwayo Utopia kwenye mswada uitwao Republika. Hii ilikuwa miaka 375 kabla kuzaliwa kwa Yesu.

Tangu zama hizo, wanasiasa wameibuka kuwa mabingwa wa kubuni nchi iitwayo Utopia kisha kurai wananchi kuzama kwenye hadaa hizo. Leo ni miaka 2021 baada ya kuzaliwa kwa Yesu na wanasiasa nchini Kenya hawajabadili hata punje kutoka kwa simulizi za Utopia.

Kila uchao tunapata maelezo mapya kuhusu safari hii na kuacha kila mmoja wetu akiwa hoi kwa matumaini ya kusafiri kwelekea nchi ya asali na starehe isiyo na kifani. Utopia ni nchi isiyo na dosari hata kidogo. Tutakapofika huko, shida na mateso tunayoshuhudia kwa sasa vitaisha. Vilevile, Distopia ni kinyume chake.

Ukipiga darubini kwenye uhalisia wa mienendo ya wanasiasa wengi, utakubaliana na wasomi wa filosofia ya siasa kwamba, katika kila hali na muktadha kwenye jamii, wanasiasa hutafuta fursa mwafaka ya kubingirisha gurudumu la maslahi yao kwa kuzua na kujenga taswira ya mambo mawili Utopia na Distopia. Yaani kwa ushawishi wa vinywa vyao, wachuuzi hawa wa siasa wanatuuzia tu mambo haya mawili. Aidha tuchague Utopia yao ambako ni raha isiyo na kifani au tuambulie kwenye Distopia ya wapinzani wao ambako ni karaha, mateso na maangamizi ya ajabu. Wanasiasa wa Kenya ni mabingwa katika kutuandalia makao kwenye taifa liitwalo Utopia! Wakati huo huo, wanatumia mbinu ya vitisho na hofu ili tusichague kingine isipokuwa maono yao. Raia nao ni kielelezo cha kila aina ya sarakasi, wakati mwingine ujinga mkuu, kwa kuamini uwepo wa safari hii na kuunga mkono utapeli wa hawa ‘wachuuzi wa Utopia’. Ndio maana ghasia hutokea kila tunapokaribia uchaguzi mkuu.

Katika Utopia ya Plato; viongozi wana hekima ya malaika na juhudi zao ni kuangamiza njaa, kiu na uhaba wa kila aina. Utopia haina maskini na kila kiumbe ana haki na usawa. Utopia haina dhuluma na raia hawajihusishi na vita. Utopia ya Wakenya hubadilika kila baada ya miaka mitano.

Tunaahidiwa maisha ya peponi kwa kuonjeshwa moto wa jehanamu. Ilivyo sasa tumeanza miereka kati utopia na distopia kuhusu mwaka wa 2022. Utopia ya sasa imeundwa kwa ahadi za ajabu za BBI kwa upande mmoja na ndoto potovu za Hustler kwa upande wa pili. Dawa ya ujinga wa wakenya ni kuerevuka na kufahamu kwamba hekaya za utopia, ni hekaya tu.

mauyaomauya@live.com

Habari zinazohusiana na hii