Fundi mjengo afichua siri kali ya buda

Na NICHOLAS CHERUIYOT

GELEGELE, SOTIK

KULIKUWA kioja katika boma moja la hapa fundi mmoja alipofika na kumdai buda malipo baada ya kumjengea kimada wake nyumba.

Duru zasema hali ilikuwa shwari katika boma la buda hadi fundi alipofika akihema, nyundo mkononi.

Buda alijua siri zake zingefichuliwa na akamsihi fundi atulie ili watatue mambo hayo.

“Mimi najua maneno yako kabisa na ninataka ukae hapa ili upewe kopo la chai kisha tuongee na kuelewana kama wanaume. Kila tatizo lina suluhu,” mzee akamlilia fundi.

“Eti nipewe chai? Unadhani utanibembeleza kwa kunipa chai? Sahau! Nilimaliza kazi kitambo na hadi sasa umekuwa ukinihepa ili usilipe deni langu. Utajua hujui,” fundi akazusha kwa uchungu.

Mke wa buda aliyekuwa akifuatilia tukio kwa ukaribu sana alitaka kujuzwa kulikoni.

“Nini kinaendelea hapa? Umetujengea nini na ni wapi hapo? Acha kupayuka ovyo, nieleze kuhusu deni hilo,” mama akasema.

“Leo ni leo, nitasema kila kitu. Huyu jamaa ana kimada mbali na hapa na alinituma nimjengee nyumba akiniahidi kunilipa lakini amedinda kufanya hivyo,” fundi alipasua mbarika na kushangaza mwanamke huyo.

Kisanga kilizidi buda na mke waliporushiana cheche za maneno huku fundi akisubiri kumkaba koo jamaa alipe deni.

“Hata huyo msichana ni yule ulinishauri nikae mbali naye lakini ibilisi alinihadaa nikamfanya awe mpenzi kwa muda mfupi tu. Kwa sasa amenitema hata,” jamaa alijitetea.

Hatimaye, buda alimlipa fundi kwa kumtumia pesa kwa simu naye jamaa akaondoka akiwa amewasha moto wa majibizano kati ya mke na mumewe.