Wakazi Lamu wapendekeza barabara na vichochoro kupewa majina maalum

Na KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa mji wa kale wa Lamu wanaishinikiza serikali ya kaunti hiyo kupeana majina kwa barabara na vichochoro vya mji huo ili kuzuia wageni na watalii kupotea wanapozuru mji huo wa kihistoria.

Ni barabara chache, ikiwemo ile ya Harambee iliyoko katikati ya mji wa Lamu ambazo zimebandikwa majina maalum.

Wakizungumza na wanahabari Ijumaa, wakazi wamesema wanaamini majina ya kutambulisha barabara na vichochoro ni wazo mwafaka litakalosaidia watalii na wageni wengine wanaozuru Lamu kuifahamu zaidi Lamu na mitaa yake.

Mji wa Kale wa Lamu ni miongoni mwa maeneo machache yanayotambulika ulimwenguni kwa kuhifadhi mila na desturi za zamani.

Mnamo 2001, Shirika la Umoja wa Mataifa Kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) liliorodhesha mji wa Lamu kuwa sehemu iliyodumisha ukale wake, yaani Unesco World Heritage Site.

Wakazi wamependekeza kuwa majina yatakayopewa barabara na vichochoro sharti yawe majina yanayoonyesha ukale wa Lamu.

“Tungeomba kaunti kufikiria kuzipa hizi barabara na vichochoro vyetu hapa Lamu majina maalum. Tunataka majina ya kale kama vile Habib Swaleh, Fumo miongoni mwa mengine ili kusaidia kutambua kwa urahisi mitaa na mila yetu,” akasema Bw Mohamed Alwy.

Bi Halima Bakari alisema kupeanwa kwa majina kwa barabara na vichochoro vya Lamu ni hatua itakayosaidia kuvutia zaidi wageni wanaozuru Lam una pia kuuza sera za kutalii wa kisiwa cha Lamu kwenye mataifa ya nje.

“Ikiwa vicbochoro na barabara zetu zitapewa majina ya kale na ya kihiostoria, naamini watalii watavutiwa zaidi kuja Lamu kujionea majina hayo ya kale na pengine kujifunza kitu hiki au kile,” akasema Bi Bakari.

Mkazi mwingine aliyeunga mkono maoni hayo ni Faris Kale.

Mkazi wa Lamu, Faris Kale. Picha/ Kalume Kazungu

Mbali na upeanaji wa majina kwa barabara na vichochoro, wakazi pia waliishinikiza kaunti kudhibiti mambo mengi ya kisasa ambayo yanaendelea kupoenyezwa kwenye mji huo wa kihistoria, hivyo kudidimiza matumaini ya ukale kudumishwa mjini humo.

Baadhi ya mambo ambayo ni kero kwa uhifadhi wa utamaduni wa mji wa kale wa Lamu ni matumizi ya usafiri wa kutumia pikipiki, ambapo zaidi ya wahudumu 300 wa pikipiki wanaendeleza shughuli ndani yam ji wa kihistoria wa Lamu kwa sasa.

Vibanda ambavyo vinaendelea kujengwa mbele ya ufuo wa Lamu pia vinaharibu hadhi ya kale yam ji huo.

Wakazi pia wametaja mavazi ya kisasa kuwa jambo linalofaa kutiliwa shaka endapo tamaduni na ukale wa Lamu utastahili kuendelezwa.

Kisiwa cha Lamu ni kimojawapo cha vivutio vya watalii wanaozuru eneo hilo.

Zaidi ya wakazi 10,000 huishi kwenye mji wa kale wa Lamu.

Habari zinazohusiana na hii