• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
Chama cha ODM chaunga mgombea wa Wiper katika uchaguzi mdogo Machakos

Chama cha ODM chaunga mgombea wa Wiper katika uchaguzi mdogo Machakos

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha ODM kimetangaza rasmi kuwa kinaunga mkono mgombea wa Wiper katika uchaguzi mdogo wa useneta wa Machakos Agnes Kavindu Muthama.

Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Ijumaa chama hicho kinapuuzilia mbali uvumi unaoenezwa mitandaoni kwamba kinaunga mkono mgombeaji wa chama cha Maendeleo Chap Chap (MCC) John Mutua Katuku.

ODM imesema kuwa Wiper imekuwa mshirika wake wa karibu katika NASA na mpango wa maridhiano (BBI).

“Kwa moyo wa BBI na NASA, chama cha ODM kimeamua kuunga mkono mgombea wa chama cha Wiper Agnes Kavindu kuwa Seneta wa Machakos,” imesema sehemu ya barua hiyo iliyotumwa kwa vyombo vya habari na mkurugenzi wake wa mawasiliano Philip Etale.

ODM inasema kuwa Bi Kavindu alichangia pakuwa katika mpango wa BBI kama mwanachama wa jopokazi la awali na baadaye akahudumu kama mwanachama wa kamati simamizi iliyoandaa mswada wa marekebisho ya katiba kupitia BBI.

Mswada huo sasa umewasilishwa kwa mabunge 47 ya kaunti baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kubaini kuwa umeungwa mkono na wapigakura 1.42 milioni waliosajiliwa.

Uchaguzi huo mdogo wa useneta wa Machakos utafanyika mnamo Machi 23 ambapo wagombea 15 watapambana.

Kando na Bi Kavindu na Bw Katuku, wagombea wengine ni; Urbanus Mutunga Muthama, almaarufu Ngengele, anayewania kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto, Mwanzia Lily Nduku (Chama cha Uzalendo), Otto Edward Musembi (Ford Asili), Joseph Mathuki (mgombea wa kujitegemea) miongoni mwa wengine.

You can share this post!

Diwani akanusha madai kuwa anachochea uhasama Kapedo

Chepkwony, Cheruto na Naibei kufufua uhasama wao kwenye...