• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 8:55 AM
Kiungo wa Santos Soccer aonyesha dalili za kuwa staa wa maana

Kiungo wa Santos Soccer aonyesha dalili za kuwa staa wa maana

Na PATRICK KILAVUKA

KIUNGO Nancy Nafula,19, mwanafunzi wa Kidato cha Tatu Shule ya Upili ya Dagoretti Mixed, Gatina, Kawangware na wa zamani wa Shule ya Msingi ya Muslim, Kawangware anaendelea kujitahidi kulea kipawa chake cha soka uwanjani akiwa katika timu ya mtaani ya Santos Soccer yenye maskani uwanjani wa NCC, Dagoretti Corner, Nairobi.

Amezaliwa katika familia ya uhitaji japo utajiri wa kipaji anao hali ambayo imempelekea kupata ufadhili wa masomo na kudumisha mizizi ya kipawa chake cha kandanda.

Kiungo Nafula anapocheza ugani, hapo ndiposa unangamua kuwa kitabu hakihukumiwa kwa ukurusa wa juu.

Kiungo huyo ni mchezaji ambaye anachonga na kumega pasi mithili ya fundi mchongezi. Ana chenga za maudhi na akipata nafasi ya kujaza kimiani huwa radhi kuduwaza makipa!

Kukolea kwa kipaji kumemwezesha kiungo huyo mvamizi kupeperusha bendera ya mashindano ya Copa Coca Cola kwa wasiozidi miaka kumi na sita, mwaka wa 2017, akiwa shule ya msingi hadi kitaifa.

Mwaka 2020 alishiriki katika timu ya Shule ya Upili ya Dagoretti Mixed japo katika fainali za kitaifa ambazo zilifanyika Kisumu, alikuwa na jeraha ambalo lilimuingiza katika ulazima wa kukaa benchi.

Hata hivyo anasema mwakani yuko ngangari kuonyesha kwamba kuvunjika kwa mwiko si mwisho wa kupika.

Kiungo Nancy Nafula wa timu ya akina dada ya Santos Soccer akipepeta mpira. Picha/ Patrick Kilavuka

Katika kujiimarisha kitalanta, aliamua kusaka majani mabichi katika timu ya mtaani ya Santos Soccer mwaka 2020 ambayo inafanyia mazoezi uwanja wa manispaa ya Nairobi, Dagoretti Corner (NCC ). Alikuwa tegemeo wa timu hiyo katika kipute cha Westlands Soka Association baada ya kufika fainali ingawa ilibanduliwa na Kibagare Girls kwa matuta 4-2.

Je, alijiunga Santos kivipi? Kulingana na kocha wa timu hiyo Devis Ekocheli almaarufu ‘Asuka’ anasema Nafula alikuwa na uraibu wa kufanya mazoezi na timu ya wavulana kabla kubuniwa ya akina dada.

“Nilimjua kupitia uraibu wake wa kujinoa kila mara akionyesha uwezo wake wa kucheza mbele ya wavulana kwa ukakamavu, ujasiri, nidhamu ya juu na kuwa mfuata maagizo kwa njia mufti na mchezo wake ukawa wa kuimarika kila uchao. Isitoshe,mazoezini, aliibuka kuwa mchezaji hodari na tegemeo,” asema kocha huyo ambaye amewahi kumpeleka katika majaribio ya Harambee Starlets ya wasiozidi miaka ishirini japo hakufua dafu kwa wakati huo. Ingawa hivyo, anasema alijifunza mawili matatu ya kupiga kampeni za siku zijazo.

Mchezaji ambaye humfurahisha kutokana na uchezaji wake ni Cristiano Ronaldo wa Juventus kutokana na mbwembwe zake za chenga maridadi, bidii, nidhamu na uwiano wake uwanjani. Hata hivyo, timu yake anayoshabikia ni Real Madrid.

Kutokana na uelewa wa mchezo na kuamini kwamba anaweza kufika mbali na wazazi wake kumshika mkono kuinua kiwango cha uchezaji wake, amejitia hamnazo za ufanisi na faraja.

“Himizo zao zinanifariji na kunipa moyo wa kuendeleza maono yangu katika fani hii,” anasema mchezaji huyo wa safu ya kati ambaye anatarajia mengi mema huku akiwashauri mabinti wengine kwamba, kabumbu yaweza kuwafikisha mbali katika maisha kwani anaamini soka inalipa kitaifa na kimataifa kutokana na wachezaji ambao wametambulika nchini na ughaibuni.

Isitoshe, kuna ufadhili wa masomo na “unaweza kukutoa mavumbini.”

Changamoto yake ni buti, jezi na usafiri.

You can share this post!

AKILIMALI: Mboga zinaweza kukaushwa zitumike wakati wa...

Mwendwa aidhinishwa kuwania nafasi ya haiba katika Baraza...