Wambora achaguliwa mwenyekiti wa CoG

CHARLES WASONGA na STEVE OTIENO

GAVANA wa Embu Martin Nyaga Wambora sasa ndiye Mwenyekiti mpya wa Baraza la Magavana Nchini (CoG).

Bw Wambora amechukua mahala pa mwenzake wa Kakamega, Wycliffe Oparanya ambaye amekamilisha mihula yake miwili.

Bw Wambora wa chama cha Jubilee na anayehudumu muhula wa pili kwa ugavana, alichaguliwa jana asubuhi jijini Nairobi.

Uchaguzi huo uliendeshwa kwa njia ya maelewano ingawa magavana Dhadho Godhana (Tana River) na Charity Ngilu (Kitui) pia walikuwa wakimezea mate kiti hicho.

Baraza hilo halijawahi kuwa na mwenyekiti wa kike.

Gavana wa Kisii, James Ongwae (ODM) alichaguliwa kuwa Naibu Mwenyekiti naye Gavana wa Elgeyo Marakwet, Alex Tolgos ndiye kiranja mpya.

Katika hotuba yake fupi, Bw Wambora aliahidi kutetea kuongezwa kwa mgao wa fedha kwa kaunti na kutolewa kwa fedha hizo kwa wakati ufaao.