• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Rais akerwa na utovu wa nidhamu shuleni

Rais akerwa na utovu wa nidhamu shuleni

Na NICHOLAS KOMU

RAIS Uhuru Kenyatta ameagiza Wizara ya Elimu kuchunguza chanzo cha utovu wa nidhamu shuleni na kubuni suluhisho la kudumu.

Kiongozi wa taifa ambaye yuko ziarani katika eneo la Kati, ametoa wito kwa wadau wote katika sekta ya elimu kujadiliana kuhusu jinsi ya kukomesha visa vya kuteketeza na kususia shule.

Msemaji wa Ikulu, Bi Kanze Dena alisema rais anafuatilia kwa makini vurugu ambazo zimekumba shule hasa za sekondari.

“Vurugu hizo ni suala tata mno na rais anafuatilia hali hiyo kwa makini. Ameapa kufikia kiini na kuagiza Wizara ya Elimu na wadau husika kuchuguza suala hilo na kutafuta suluhisho,” alisema.

Rais pia ametoa wito kwa marafiki na wadau kuunga mkono serikalli katika uboreshaji wa miundomsingi shuleni katika juhudi za kuwezesha wanafunzi kuzingatia kanuni za afya kuhusu Covid-19.

Tangu masomo yaliporejelewa mapema mwaka huu wa 2021, shule zimekuwa ziking’ang’ana kutekeleza masharti ya afya hususan kuweka umbali, huku shule zikikosa miundomsingi ya kutosha.

Hali hii imesababisha shule nyingi kushindwa kuwalinda watoto dhidi ya maambukizi huku wengine wakilazimika kusomea chini ya miti.

“Rais ametoa wito kwa marafiki wa Kenya na washikadau kujitokeza ili kuhakikisha kwamba watoto wanaendelea na masomo yao ipasavyo,” ilisema Ikulu.

Aidha, serikali imesema mikakati yote itatekelezwa ili kuhakikisha watahiniwa wanaotazamiwa kufanya mitihani yao katika muda wa miezi mitatu wanakalia hivyo bila tatizo.

Haya yatafanikishwa kwa kuweka mikakati ya kiafya na kiusalama ya kuwalinda wanafunzi wanapofanya mitihani na pia kuhakikisha raslimali zote zinapatikana.

Pia wanafunzi wajawazito wataruhusiwa kuendelea na masomo yao pindi watakapojifungua.

Mapema 2021 serikali iliagiza mamia ya watoto wa shule waliopachikwa mimba wakati wa likizo ndefu kuruhusiwa kurejea shule.

You can share this post!

Washukiwa saba, silaha 35 zanaswa katika operesheni...

Uhuru na Raila mbioni kuokoa BBI ngome zao