• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 5:29 PM
Uhuru na Raila mbioni kuokoa BBI ngome zao

Uhuru na Raila mbioni kuokoa BBI ngome zao

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, wako mbioni kuokoa mchakato wa marekebisho ya Katiba wa BBI katika ngome zao za kisiasa za Mlima Kenya na Nyanza, mtawalia.

Hii ni baada ya mchakato huo kukabiliwa na mawimbi makali ya upinzani haswa kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kisiasa na wa kidini wakati ambapo mswada wa BBI umewasilishwa katika mabunge 47 ya kaunti.

Leo Jumamosi Rais Kenyatta anaongoza mkutano wa viongozi wa matakaba mbalimbali katika Ikulu ndogo ya Sagana kujadili mikakati ya kuvumisha BBI, wakati ambapo wabunge zaidi ya 40 kutoka Mlima Kenya wameonya kwamba haitakuwa rahisi kwa mswada huo kupata umaarufu eneo hilo.

Bw Odinga ameitisha mkutano wa viongozi wa kaunti za Luo Nyanza mjini Kisumu mnamo Februari 8, kujadili mipango ya kupitisha mswada wa BBI katika mabunge ya kaunti hizo nne za Homa Bay, Siaya, Kisumu na Migori.

Walioalikwa katika mkutano huo, ambao utafanyika katika mkahawa wa Ciala Resort, ni wabunge, maseneta, magavana, madiwani na wanachama wa kamati za kushirikisha shughuli za ODM katika kaunti zote nchini.

Wengine walioalikwa ni wanachama wa Baraza la Wazee, wataalamu na wafanyabiashara kutoka kaunti husika.

“Kila kaunti itawakilishwa na ujumbe usiozidi watu 200. Gavana Anyang’ Nyong’o atawasiliana na kila ujumbe kupitia kwa magavana wao ili kuwapa maelezo zaidi kuhusu mkutano huo utakaoongozwa na Kiongozi wa ODM Mhe Raila Odinga,” ikasema taarifa ya mwaliko iliyotolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho Edwin Sifuna.

Ijumaa, Rais alikutana na madiwani kutoka eneo la Kati, ambao baada ya mkutano wao waliahidi kupitisha Mswada wa marekebisho ya katiba haraka iwezekanavyo.

Mapema wiki hii, alikuwa amekutana na magavana wa eneo hilo katika Ikulu ya Nairobi.

Madiwani takriban 550 waliotoa hakikisho hilo kwa Rais Kenyatta wanatoka kaunti za Meru, Tharaka Nithi, Embu, Kirinyaga, Nyeri, Murang’a, Nyandarua, Kiambu, Laikipia na Nakuru.

Rais alisisitiza kwamba urekebishaji Katiba utasaidia kupunguza uhasama wa kisiasa na kuhakikisha ugavi sawa wa rasilimali za umma kitaifa.

“Ni wajibu wetu kama viongozi kuhakikisha tunatenda haki na wala si kutishia au kutusi wengine. Tunahitaji kuhakikisha kwamba kuna haki na maendeleo kwa wananchi waliotuchagua,” akasema Rais.

Mswada huo unapendekeza kuwa serikali za kaunti zitapokea mgao usiopungua asilimia 35 wa mapato ya kitaifa ambapo asilimia 5 ya mgao huo itatumiwa kufadhili miradi ya maendeleo katika ngazi za wadi.

Kwa wastani kila wadi inakadiriwa kupokea Sh22 milioni za maendeleo kupitia Hazina ya Ustawi wa Wadi itakayosimamiwa na madiwani. Pendekezo hilo linasemekana kuwa “chambo” cha kuwavutia madiwani kupitisha mswada huo ambao unahitaji kupitishwa na angalau mabunge 24 ya kaunti kabla ya kuwasilisha katika Bunge la Kitaifa na Seneti.

Hata hivyo, Naibu Rais William Ruto na wabunge wandani wake wamepuuzilia mbali ahadi hiyo wakisema serikali haiwezi kuimudu.

You can share this post!

Rais akerwa na utovu wa nidhamu shuleni

Rais Kenyatta njia panda akikutana na viongozi Mlimani leo...