Rais Kenyatta njia panda akikutana na viongozi Mlimani leo Jumamosi

Na WANDERI KAMAU

WAKENYA wameelekeza macho yote kwa Rais Uhuru Kenyatta kuona ikiwa ataweza kuhimili baadhi ya changamoto za kisiasa na kiuchumi zinazomkabili anapojitayarisha kung’atuka kutoka uongozini mwaka 2022.

Jumamosi hii, Rais Kenyatta anatarajiwa kukutana na viongozi kutoka ukanda wa Mlima Kenya katika Ikulu Ndogo ya Sagana, Kaunti ya Nyeri kujaribu kuwarai kumsaidia kuipigia debe ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) katika eneo hilo.

Wenyeji wamegawanyika pakubwa kuhusu ripoti hiyo, baadhi wakisema si suala la dharura linalopaswa kuangaziwa na serikali. Wanasisitiza Rais anapaswa kushughulikia masuala yenye uzito kama hali mbaya ya uchumi na kudorora kwa sekta muhimu kama kilimo.

Masuala mengine yanayoonekana kumwandama Rais Kenyatta ni wasiwasi wa ODM kuhusu utekelezaji wa handisheki, kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, madai ya migawanyiko miongoni mwa washirika wake wakuu serikalini na katika kundi la ‘Kieleweke’ ambalo limekuwa likimpigia debe kati ya mengine.

Chini ya mazingira hayo, wadadisi wanasema Rais Kenyatta ana nafasi ndogo sana kufanya maamuzi ambayo yatabadilisha hali ya siasa nchini.

Kulingana na Bw Javas Bigambo, ambaye ni mdadisi wa siasa, Rais Kenyatta hana muda wa kutosha hata kidogo.

“Rais hana muda. Kuhusu suala la uchumi, hana muda kubadilisha hali. Uchumi hauwezi kulazimishwa kuimarika sasa kutokana na changamoto zinazotokana na athari za janga la virusi vya corona. Kiwastani, itachukua kati ya miaka mitatu na mitano uchumi kurejea kiwango ulichokuwa kabla ya janga la corona,” akasema Bw Bigambo kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo.’

Tangu alipochukua uongozi mnamo 2013, Rais Kenyatta amekuwa akilaumiwa kutokana na ongezeko la deni la kitaifa.

Ingawa serikali yake imekuwa ikijitetea inaelekeza fedha hizo kwenye miradi ya maendeleo, mingi imekuwa ikikumbwa na sakata za ufisadi kama vile ujenzi tata wa mabwawa ya Arror na Kimwarer. Inadaiwa serikali ilipoteza zaidi ya Sh19 bilioni kwenye sakata hiyo. Kenya pia inakisiwa kuwa na deni la nje la zaidi ya Sh7 trilioni.

BBI

Kwenye juhudi zake kutuliza joto Mlima Kenya, wadadisi wanasema bado itakuwa vigumu kuwarai wenyeji kubadilisha msimamo wao kisiasa, hasa ikizingatiwa hawanii urais 2022.

Katika kikao cha Sagana, Rais Kenyatta anatarajiwa kuwarai viongozi kumsaidia kuendeleza ngoma kuhusu BBI, ambayo imezua hisia mseto katika eneo hilo.

Kulingana na Bw Bigambo, njia pekee aliyo nayo Rais ni kuhakikisha eneo limepata mgao mkubwa wa fedha kwenye bajeti ya mwaka 2021/22, kwani ndiyo itakayokuwa ya mwisho kwenye utawala wake.

“Kimsingi, hiyo ndiyo njia ambayo anaweza kuwaridhisha wenyeji. Hata hivyo, hilo bado ni ngumu kutimiza kwani kuna taratibu ambazo lazima zifuatwe katika kuhakikisha kila sekta imepata mgao wake wa fedha kwa mujibu wa kanuni zilizo kwenye sheria,” akasema Bw Bigambo.

Profesa Macharia Munene, ambaye pia ni mdadisi wa siasa, anasema kuwa njia ya pekee ambayo Rais huenda akapunguza uasi unaomkabili ni kukubali hisia zinazotolewa na mirengo yote ya kisiasa badala ya kutoa vitisho.

Rais Kenyatta amekuwa akitoa na maonyo makali, akionekana kuwalenga wanasiasa wanaoegemea mrengo wa ‘Tangatanga’ unaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto kwenye azma yake kuwania urais 2022.

“Rais anapaswa kuanza kuwa mvumilivu. Lengo kuu ni kuhakikisha amedumisha taswira ya taasisi ya urais kama ishara ya umoja wa kitaifa. Vile vile, anapaswa kukoma kuonekana kuwapendelea baadhi ya viongozi hadharani,” asema Prof Munene.

Hapo Jumanne, Rais Kenyatta alisisitiza kuwa bado yu mamlakani, na hakuna kiongozi yeyote anapaswa kuhisi kama kuna pengo la uongozi nchini.

Kwenye mahojiano na vituo vya redio vinavyopeperusha matangazo yake na lugha ya Gikuyu, Rais alisema ameanza mikakati kutimiza ahadi alizotoa kwa Wakenya, akieleza imani kuzitimiza kabla ya muhula wake kuisha.

“Mimi niko kazini. Mawaziri yangu pia wako kazini. Tunataka kuhakikisha tumetimiza yale tuliahidi Wakenya. Hiyo ndiyo sababu sionekani sana,” akasema.

Wataalamu wa masuala ya kiuchumi wanasema muda uliobaki ndio utaamua sifa ambayo Rais ataacha kwa wakati ambao amehudumu kama rais tangu 2013.

“Huu ni wakati ambao Rais Kenyatta anapaswa kuutumia vyema. Ndio utaamua ikiwa atarejesha imani kwa Wakenya au la. Ni wakati anaopaswa kuutumia kuondoa vikwazo vyovyote vinavyomkabili,” asema Tony Wetima, ambaye ni mdadisi wa masuala ya uchumi.

Habari zinazohusiana na hii

Uhuru aomba talaka

NDIO! HAPA WIZI TU

Ahadi juu ya ahadi

Huu ni mzaha tu!